94. Sura ya pili: Kudhihiri kwa Bid´ah katika maisha ya waislamu

Kudhihiri kwa Bid´ah katika maisha ya waislamu. Chini yake kuna masuala yafuatayo:

Masuala ya kwanza: Wakati Bid´ah ilipodhihiri. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema[1]:

“Tambua kwamba Bid´ah kwa ujumla wake zinazofungamana na elimu na ´ibaadah zilijitokeza katika Ummah mwishoni mwa zama za makhaliyfah waongofu, kama alivoelezea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Yeyote atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu”.”

Bid´ah ya kwanza kujitokeza ni Bid´ah ya Qadar, Bid´ah ya Irjaa´, Bid´ah ya Tashayyu´ na Khawaarij. Wakati kulipotokea mpasuko kwa kuuawa kwa ´Uthmaan ndipo kukajitokeza Bid´ah ya Haruuriyyah. Halafu mwishoni mwa kipindi cha Maswahabah ndipo wakajitokeza Qadariyyah mwishoni mwa zama za Ibn ´Umar, Ibn ´Abbaas, Jaabir na Maswahabah wengine mfano wao (Radhiya Allaahu ´anhum). Karibu na wakati huo wakajitokeza pia Murji-ah. Ama Jahmiyyah walijitokeza mwishoni mwa zama za Taabi´uun baada ya kufariki ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz. Imepokelewa kwamba aliwaonya. Jahm alijitokeza  Khuraasaan katika uongozi wa Hishaam bin ´Abdil-Malik.”

Bid´ah hizi zilijitokeza katika karne ya pili na Maswahabah wakiweko na  wakawakaripia wenye nazo. Kisha ikajitokeza Bid´ah ya I´tizaal, kukatokea fitina kati ya waislamu na kukajitokeza tofauti, maoni mbalimbali na kumili katika Bid´ah na matamanio. Kukajitokeza Bid´ah ya Taswawwuf na Bid´ah ya kujenga juu ya makaburi baada ya kumalizika karne bora. Hali itaendelea hivi kila ambavo zama zinavyozidi kusonga mbele ndivo Bid´ah zitaongezeka na kujitokeza kwa aina mbalimbali.

Masuala ya pili: Miji ya Kiislamu inatofautiana juu ya kudhihiri Bid´ah ndani yake. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Miji mikubwa waliyoishi ndani yake Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na elimu na imani ikatoka ndani yake ni mitano: Makkah na Madiynah, ´Iraaq mbili na Shaam na ndani yake ndiko kumetoka Qur-aan, Hadiyth, Fiqh na ´ibaadah na yenye kufuatia hayo katika mambo ya Uislamu. Katika miji hiyo kukajitokeza Bid´ah za kimsingi kusipokuwa Madiynah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuufah kulijitokeza Tashayyu´ na Irjaa´ na baada ya hapo zikaenea kwenginepo. Baswrah kujitokeza Qadar, I´tizaal na ´ibaadah mbovu. Baada ya hapo zikasambaa kwengine. Shaam kulikuweko Naswb na Qadr. at-Tajahhum ilitokea pande za Khuraasaan. Hiyo ndio Bid´ah ovu zaidi.

Kujitokeza kwa Bid´ah kulikuwa kwa kutegemea na namna watu wanavyojiweka mbali na nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya kujitokeza mpasuko kwa kuuawa kwa ´Uthmaan ndipo ikajitokeza Bid´ah ya Haruuriyyah. Kuhusu mji wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulikuwa umesalimika kutokeza Bid´ah hii ingawa walikuweko wenye kulificha jambo hilo. Mtu sampuli hiyo alikuwa ni mwenye kutwezwa na mwenye kusemwa vibaya anapojitokeza mtu katika Qadariyyah na wengineo. Lakini walikuwa ni wenye kukandamizwa na wenye kudhalilishwa. Tofauti na Tashayyu´, Irjaa´ huko Kuufah, I´tizaal, Bid´ah ya kuabudu huko Baswrah na Naswb huko Shaam. Bida´ah hizi zilikuwa waziwazi. Isitoshe imethibiti katika “as-Swahiyh” kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba ad-Dajjaal hatoingia ndani yake. Bado elimu na imani viko waziwazi mpaka katika  zama za wanafunzi wa Maalik, ambao walikuwa miongoni mwa watu wa karne ya nne.”[2]

Katika zile karne tatu bora Madiynah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukuwepo kabisa Bid´ah za waziwazi na hakukujitokeza Bid´ah kabisa katika misingi ya dini kama zilivyojitokeza katika miji mingine.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/354).

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (20/300-303).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 184-186
  • Imechapishwa: 02/07/2020