Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapotaka kuomba dhidi ya mtu au kumuombea mtu basi huleta Qunuut[1] katika ile Rak´ah ya mwisho baada ya Rukuu´ baada ya kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah anamsikia yule mwenye kumhimidi.”

na:

اللَّهُمَّ رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ

“Ee Allaah! Mola wetu! Na himdi zote ni Zako.”[2]

Anasoma Qunuut kwa sauti ya juu[3] na ananyanyua mikono[4]. Waswaliji nyuma yake husema:

آمين

“Aamiyn.”[5]

Alisoma (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Qunuut katika swalah zote tano[6]. Lakini hata hivyo alikuwa hasomi Qunuut ndani yake isipokuwa kama anataka kumuombea mtu au kuomba dhidi ya mtu[7]. Wakati mwingine huenda akasema:

“Ee Allaah! Muokoe al-Waliyd bin al-Waliyd, Salamah bin Hishaam na ´Ayyaash bin Abiy Rabiy´ah. Ee Allaah! Muadhibu vikali Mudhar na mfanye akutane na miaka kama aliyokutana nayo Yuusuf. [Ee Allaah! Mlaani Lihyaan, Ri´l, Dhakwaan na ´Uswayyah ambao wamemuasi Allaah na Mtume Wake.]”[8]

Pindi anapomaliza kuleta Qunuut husema:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

kisha anasujudu[9].

[1] Qunuut inaweza kuwa na maana nyingi. Makusudio hapa ni du´aa ndani ya swalah sehemu maalum.

[2] al-Bukhaariy na Ahmad.

[3] al-Bukhaariy na Ahmad.

[4] Ahmad na at-Twabaraaniy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Ahmad na Ishaaq wanaona kuwa mikono inatakiwa kunyanyuliwa wakati wa Qunuut, kama alivyopokea al-Marwaziy katika “al-Masaa-il”, uk. 23. Lakini haikupokelewa jambo la kufuta uso sehemu hii na hivyo kitendo hicho ni Bid´ah. Ama kuhusu kupangusa nje ya swalah, haikusihi kupokelewa. Kumepokelewa tu Hadiyth dhaifu juu ya hilo na baadhi ni dhaifu zaidi kuliko zengine, kama nilivyothibitisha katika ”Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud” (262) na ”Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (597). Kwa ajili hiyo al-´Izz bin ´Abdis-Salaam amesema katika baadhi ya fatwa zake:

“Hakuna wanaofanya hivo isipokuwa tu wajinga.”

[5] Abu Daawuud na as-Sarraaj. al-Haakim ameisahihisah na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[6] Abu Daawuud, as-Sarraaj na ad-Daaraqutwniy kwa cheni mbili za wapokezi zilizo nzuri.

[7] Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” (1/78/2) na al-Khatwiyb katika ”Kitaab-ul-Qunuut” kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[8] Ahmad na al-Bukhaariy. Nyongeza imepokelewa na Muslim.

[9] an-Nasaa’iy, Ahmad, as-Sarraaj (1/109) na Abu Ya´laa katika ”al-Musnad” kwa cheni ya wapokezi nzuri.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 155-156
  • Imechapishwa: 08/01/2019