93. Dalili ya hajj katika Qur-aan


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya hajj ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

”Kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo wa kuiendea. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni mkwasi kwa walimwengu.”[1]

MAELEZO

Mayahudi walidai kuwa ni waislamu na kwamba wanafuata dini ya Ibraahiym. Ndipo Allaah (Jalla wa ´Alaa) akawatahini katika Aayah na akasema:

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

”Kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo wa kuiendea. Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni mkwasi kwa walimwengu.”

Mkiwa kweli ni waislamu basi hijini kwa sababu Allaah amefaradhisha hajj juu ya waislamu. Msipohiji na mkaikataa hajj basi ni dalili kwamba nyinyi sio waislamu na si wenye kufuata mila ya Ibraahiym:

وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

“Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni mkwasi kwa walimwengu.”

Kwa ajili ya Allaah… – Bi maana hii ni faradhi, haki na wajibu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) juu ya watu.

Hajj – Maana yake katika lugha ni kusudio.

Maana ya hajj katika Shari´ah ni kukusudia Ka´bah tukufu na zile nembo takatifu katika wakati maalum kwa ajili ya kutekeleza ´ibaadah maalum ambayo ni zile taratibu za hajj.

Hajj katika nyumba – Bi maana Ka´bah na zile nembo zilizo pembezoni mwake ni zenye kufuatia.

مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا

“… kwa mwenye uwezo wa kuiendea.”

Hapa kunabainishwa sharti ya ulazima: kule mtu kuwa na uwezo wa kimwili na uwezo wa kimali. Uwezo wa kimwili mtu aweze kutembea, kupanda kipando na kutoka katika nchi yake na kwenda Makkah kutoka sehemu yoyote ulimwenguni. Huu ndio uwezo wa kimwili. Jambo hili halimuhusu asiyeweza kushindwa ambako ni kwa kuendelea. Kwa mfano mtu ambaye ni mgonjwa mwenye maradhi sugu yenye kuendelea na mtumzima. Watu kama hawa hawana uwezo wa kimwili. Wakiwa na uwezo wa kimali basi wanatakiwa kumuwakilisha mtu ambaye atawahijia hajj ile ya kwanza ambayo ndio faradhi.

Kuhusu uwezo wa kimali ni mtu awe na kipando – kama mfano wa mnyama, gari, ndege au meli – kitachoweza kumsafirisha. Kila kifaa kwa kutegemea na wakati. Vilevile inaweza kuhusiana kwamba yuko na mali ambayo itamuwezesha kupata kifaa hicho ili aweze kutekeleza hajj. Vilevile anatakiwa awe na akiba ya matumizi wakati wa safari yake kwenda na wakati wa kurudi. Kwa yule ambaye yuko na wanaomwangalia yeye basi anatakiwa awe na akiba ya kutosha mpaka pale ataporejea kwao. Akiba maana yake ni kwamba awe na kitu cha kumtosheleza safarini mwake na kitawatosha vilevile wale wanaomwangalia katika watoto wake, wazazi wake na wakeze na kila ambaye anamsimamia yeye. Awaachie kitachowatosheleza mpaka pale ataporejea kwao. Haya yanatakiwa kufanywa baada ya kumaliza madeni kama atakuwa ni mwenye madeni. Yakitimia haya inakuwa ndio njia: akiba na kipando kama ilivyopokelewa katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa)[2].

Asiyeweza – Asiyekuwa na akiba wala kipando basi hajj haimlazimu. Kwa sababu sio mwenye kuweza. Sharti ya ulazima wa hajj ni uwezo.

Wakati ambapo hajj ilikuwa ni yenye kuendewa kutoka kila pembe ya dunia, inahitaji matumizi, ndani yake kuna mashaka na tabu na ndani yake kunaweza kuwa khatari basi miongoni mwa rehema Zake Allaah akaifanya ni mara moja katika umri. Chenye kuzidi juu ya hapo kimependekezwa. Hii ni miongoni mwa huruma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa kutoiwajibisha kwa waislamu kila mwaka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah ameifaradhisha kwenu hajj. Hivyo hijini!” al-Aqraa’ bin Haabis (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: “Ni kila mwaka, ee Mtume wa Allaah?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamnyamazia. Kisha akamuuliza tena ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ningeitika ndio msingeweza. Hajj ni mara moja. Chenye kuzidi kimependekezwa tu.”[3]

Hii ni katika rehema ya Allaah.

وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ

“Na atakayekanusha, basi hakika Allaah ni mkwasi kwa walimwengu.”

Ndani yake kuna dalili kwamba yule mwenye kukataa kuhiji ilihali ana uwezo basi ni kafiri.

وَمَن كَفَر

“Na atakayekanusha… “

Bi maana mwenye kukataa kuhiji ilihali ni muweza wa kuhiji, basi hiyo ni kufuru. Kuna uwezekano ikawa ni kufuru ndogo. Mwenye kukataa hali ya kupinga uwajibu wake ni kufuru kwa maafikiano ya waislamu wote. Kuhusu yule mwenye kukubali uwajibu wake lakini hata hivyo akaacha kwa uvivu ni kufuru ndogo. Lakini akifa na ameacha mali basi anatakiwa kuhijiwa kutoka katika mirathi yake. Kwa sababu ni deni juu yake la Allaah (´Azza wa Jall).

Katika Aayah hii kuna ulazima wa hajj. Ni nguzo moja wapo miongoni mwa nguzo za Uislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ya Jibriyl na Hadiyth ya Ibn ´Umar amebainisha kuwa ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu.

Kuna maoni yanayosema kuwa Hajj imefaradhishwa katika mwaka wa tisa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuhiji katika mwaka huu isipokuwa alihiji katika mwaka unaofuata baada ya hapo ambao ni mwaka wa tisa. Kwa nini? Kwa sababu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) awatangazie watu katika msimu:

“Asihiji mshirikina baada ya mwaka huu na wala asitufu mtu katika Nyumba akiwa uchi.”[4]

Wakati washirikina na waliouchi walipozuia kufanya hajj katika mwaka wa kumi ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akahiji hajj ya kuaga.

[1] 03:97

[2] at-Tirmidhiy (813) na Ibn Maajah (2896).

[3] Imaam Ahmad katika ”al-Musnad” (04/151) (2304), Abu Daawuud (1721) na an-Nasaa´iy (05/111).

[4] al-Bukhaariy (369) na Muslim (1347).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 190-192
  • Imechapishwa: 19/01/2021