90. Muumini mwenye nguvu ndiye anapendwa zaidi na Allaah kuliko dhaifu


Murji-ah wanapinga na kusema haizidi na wala haipungui. Wanasema kuwa imani ni kitu kiko moyoni na ni kitu kimoja tu. Hawaoni kuwa watu wanashindana katika imani. Wanaonelea kuwa imani ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) ni sawa na imani ya mtenda dhambi mkubwa kabisa. Haya ni maneno batili. Baadhi ya waumini imani zao ni zenye nguvu zaidi kuliko wengine. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini mwenye nguvu ni bora na anapendwa zaidi na Allaah kuliko muumini dhaifu – na kwa wote wawili kuna kheri.”[1]

Inahusiana na nguvu za kiimani, za kimwili na za kimatendo.

Imani inazidi na kupungua bila ya shaka. Maasi yanaipunguza imani ilihali mambo ya utiifu yanaiongeza. Hii ndio maana ya imani kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Sema kuwa imani ni maneno… – Bi maana kutamka kwa ulimi.

… na nia – Bi maana kuamini kwa moyo

na kitendo… – Matendo ya viungo.

Kwa hivyo imani ni maneno, kuamini na matendo. Haya ndiyo yenye kufahamishwa na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama ilivyo katika Hadiyth ya tanzu za imani na nyenginezo.

Inapungua kwa maasi wakati fulani… –  Hii ni Radd kwa Murji-ah wanaosema kuwa imani haizidi na wala haipungui. Wanasema kuwa ni kitu kimoja na watu wake katika msingi wake wako sawasawa. Haya ni maneno batili. Uhalisia ni kuwa imani inazidi kwa utiifu na inashuka kwa kufanya maasi.

[1] Muslim (2667)