90. Dalili ya tafsiri ya Tawhiyd kwa mujibu wa Qur-aan


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya swalah na zakaah na tafsiri ya Tawhiyd, ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili, na wasimamishe swalah na watoe zakah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.”[1]

MAELEZO

Swalah ni nguzo ya pili katika nguzo za Uislamu. Zakaah ni nguzo ya tatu na imeambatana na swalah katika Kitabu cha Allaah. Swalah ni kitendo cha kimwili na zakaah ni kitendo cha kimali. Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Ninaapa kwa Allaah nitampiga vita mwenye kutofautisha swalah na zakaah.”[2]

Alisema hivo pindi baadhi ya watu walipokataa kutoa zakaah baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Abu Bakr aliwapiga vita na akasema:

“Ninaapa kwa Allaah nitampiga vita mwenye kutofautisha swalah na zakaah. Ninaapa kwa Allaah endapo watajizuia kunipa kimeme walichokuwa wanakitoa kumpa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi nitawapiga vita kwacho.”

Zakaah ni haki ya lazima juu ya mali. Ni nguzo moja wapo miongoni mwa nguzo za Uislamu. Ni nguzo moja wapo miongoni mwa nguzo za Uislamu. Ni kitu kimekwenda sambamba ndani ya Qur-aan katika Aayah nyingi kwa mfano:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili, na wasimamishe swalah na watoe zakaah.”

Dalili ya Tawhiyd ni katika sehemu yake ya mwanzo pale aliposema (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

 “Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.”

Hii ndio tafsiri ya Tawhiyd. Ni kule kumwabudu Allaah, pamoja na kumtakasia Yeye nia na mtu akaacha kuabudu vyenginevyo. Dini, Tawhiyd na ´ibaadah maana zake ni moja:

مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“… hali ya kumtakasia Yeye dini.”

Bi maana ´ibaadah. Hii ndio tafsiri ya Tawhiyd. Mambo si kama wanavosema wanachuoni wa falsafa kwamba ni kukubali kuwa Allaah ndiye muumbaji, mruzukaji, muhuishaji na mfishaji. Hii ni Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Lengo ni Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah waliyolingania kwayo Mitume. Muislamu hawi muislamu isipokuwa mpaka aitekeleze. Mwenye kutekeleza Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah peke yake sio muislamu. Dalili ya hilo ni kwamba washirikina walikuwa wakiiamini, wakiitamka na wakiitambua lakini hata hivyo Tawhiyd yao hii haikuwaingiza ndani ya Uislamu, haikuzuia wao kuuliwa na kuporwa mali yao. Kwa sababu hawakuwa wapwekeshaji pindi walipomshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) katika ´ibaadah. Hii ndio tafsiri ya Tawhiyd kutoka katika Qur-aan na si kutoka katika kitabu cha mtu fulani kama mfano wa kitabu “al-Jawharah”[3], “al-Mawaaqif”[4] au vitabu vyengine vya wanachuoni wa falsafa. Tafsiri ya Tawhiyd haichukuliwi kutoka katika vitabu kama hivi. Tafasiri ya Tawhiyd inachukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah na kutoka katika vitabu vya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah walioshikamana barabara na Qur-aan na Sunnah.

[1] 98:05

[2] al-Bukhaariy (1400) na Muslim (20).

[3] Kitabu ”Jawharat-ut-Tawhiyd” kinathitisha madhehebu ya Ashaa´irah. Ndani yake kuna mambo mengi yanayotofautiana na madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

[4] Kitabu ”al-Mawaaqif fiy ´Ilm-il-Kalaam” cha al-Laa-ijiy.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 186-188
  • Imechapishwa: 18/01/2021