Zakaat-ul-Fitwr ni faradhi iliyofaradhisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindipo Ramadhaan inapokwisha. ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifaradhisha kutoa Swaa’ ya tende au Swaa’ ya ngano kuwa ni Zakaatul-Fitwr iliyowajibika kwa waislamu wote; mtumwa aliye huru, mwanamume, mwanamke, mtoto mdogo na mzee na kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Chakula kinatakiwa kuwa kile kinacholiwa na watu. Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulikuwa tukitoa Zakaatul-Fitwr Swaa’ moja ya chakula, Swaa’ ya ngano, Swaa’ ya tende, Swaa’ ya mtindi mkavu au Swaa’ ya zabibu.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy.

Haijuzu kutoa Zakaat-ul-Fitwr pesa, magodoro, nguo, mifugo, samani na vinginevyo. Kwa sababu hayo yanaenda kinyume na yale aliyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, kitarudishwa kwake.”[3]

Bi maana atarudishiwa yeye mwenyewe.

Swaa´ moja ni sawa na gramu 2400 ya ngano zuri. Hiki ndio kipimo cha kiutume cha Zakaat-ul-Fitwr.

Ni wajibu kutoa Zakaat-ul-Ftwr kabla ya kwenda kuswali swalah ya ´Iyd. Bora ni kuitoa siku ya ´Iyd kabla ya swalah ya ´Iyd. Hata hivyo ni sawa kuitoa siku moja au mbili kabla ya ´Iyd. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefaradhisha Zakaat-ul-Fitwr ili mfungaji atwaharishwe na ujinga na magomvi ili kuwalisha masikini. Mwenye kuitoa kabla ya swalah basi ametoa zakaah yenye kukubaliwa na mwenye kuitoa baada ya swalah ametoa swadaqah miongoni mwa swadaqah.”[4]

Ameipokea Abu Daawuud na Ibn Maajah.

Lakini lau hakujua kuwa ni ´Iyd isipokuwa baada ya swalah au wakati wa kuitoa alikuwa kwenye sahara au mahala ambapo hakuna mwenye kuistahiki, ni sahihi akaitoa baada ya swalah ya ´Iyd pale atapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo na Allaah ndiye anajua zaidi.

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, ahli zake na Maswahabah zake.

[1] al-Bukhaariy (1503) na Muslim (984).

[2] al-Bukhaariy (1508) na Muslim (985).

[3] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[4] Abu Daawuud (1609), Ibn Maajah (1827), ad-Daaraqutwniy (2/138) na al-Haakim (1/409) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Ni Hasan kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1420).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 05/06/2017