9. Mfano wa madhambi ya Suufiyyuun waliopetuka mipaka

Ndugu wapendwa! Makusudio yetu kwa kubainisha hali ya Suufiyyuun, sio kwa kwa ajili ya kufurahia makosa yao au mzaha. Bali makusudio yetu ni kumtahadharisha kila Muislamu asije kudanganyika na chochote katika uongo wao, kuhadaika na vitimbi vyao na makosa yao.

Hakika wanachuoni wetu, tokea zamani mpaka hii leo, wametunga vitabu ambapo wameraddi upotevu wa Suufiyyah. Miongoni mwa vitabu hivo ni kitabu “Talbiys Ibliys” cha Haafidhw Ibn-ul-Jawziy aliyekufa 597 H. Sehemu kubwa ya kurasa mia tatu inahusiana na kuraddi fikira za Suufiyyah, ´Aqiydah zao, matendo yao, mavazi yao, kuruhusu kwao ala za muziki, nyimbo, kucheza pamoja na kustarehe na vijana wadogo na wavulana chipukizi n.k. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) alikuwa na juhudi kubwa kwa kuwaraddi na kuwapiga vita. Kwa ajili hii walimtesa na wakamfunga jela mpaka (Rahimahu Allaah) akafia humo jela. Kadhalika mwanachuoni Burhaan-ud-Diyn al-Baqaaiy´ aliyefariki 885 H ameandika vitabu akiwaraddi Suufiyyah. Navyo ni:

1- Tanbiyh-ul-Ghabiyy ilaa Takfiyr Ibn ´Arabiy

2- Tahdhiyr-ul-´Ibaad min Ahl-il-´Inaad bi Bid´at-il-Ittihaad

Vyote viwili vimechapishwa pamoja katika kitabu kimoja kwa uhakiki wa Shaykh ´Abdur-Rahmaan Wakiyl (Rahimahu Allaah) kwa jina “Maswray´-ut-Twaswawwuf”. Katika vitabu hivi al-Baqaaiy´ ametaja maneno ya wanachuoni ambapo wameonelea Ibn ´Arabiy na Ibn-ul-Faaridhw kuwa ni makafiri. Kadhalika ametumia dalili ya maneno na mashairi yao ambayo ndio sababu ya wanachuoni kuonelea kuwa ni makafiri.

Ndugu wapendwa! Mwanachuoni Burhaan-ud-Diyn al-Baqaaiy´ amesema mwanzoni mwa kitabu chake “Tahdhiyr-ul-Ghabiyy” akibainisha ´Aqiydah ya Ibn ´Arabiy:

“Inatakiwa ijulikane, maneno yake – yaani Ibn ´Arabiy – ni yenye kuzunguka juu ya ukomo wa vitu vyote vilivyopo kuwa ni kitu kimoja, bi maana ya kwamba hakuna kitu kilichopo zaidi ya ulimwengu huu na kuwa Allaah ni mjumuiko wa maeneo mazima ambayo yapo tu katika sehemu mbalimbali.”

Sikiliza maneno ya Ibn ´Arabiy kuhusiana na maana ya tafsiri yake ya Jina la Allaah “al-´Aliyy” (Aliye juu kabisa). Anasema:

“Miongoni mwa Majina Yake mazuri mno ni “Aliye juu kabisa”, lakini juu ya nani? Kwa vile hakuna chochote zaidi Yake… Yeye Yuko juu ya kwa Dhati Yake au kutokana na kitu gani? Ama kuhusiana na uwepo, hakika Yeye ndiye dhati ya vyote vilivyopo… “ – mpaka aliposema kuhusu Allaah – … “Yeye ndiye yule anayeonekana na aliyefichikana katika hali ya kuonekana Kwake. Hakuna yeyote anayemuona isipokuwa Yeye Mwenyewe. Hakuna kinachofichikana Kwake, kwa sababu Yuko dhahiri kwa nafsi Yake Mwenyewe, amefichikana Kwake Mwenyewe, na Yeye ndiye anayeitwa Abu Sa´iyd al-Kharraaz. Vilevile vyenginevyo katika majina ya vitu vyenye kuzuka.”[1]

Kwa mujibu wa Ibn ´Arabiy kila kitu ni Allaah na ameweka wazi kabisa ya kwamba Allaah ni Abu Sa´iyd al-Kharraaz. Abu Sa´iyd al-Kharraaz ni Suufiy wa Baghdaad aliyefariki katika mwaka wa 277 baada ya Hijrah. Ndugu! Je, maneno haya si ya khatari kuliko yale wayasemayo wakristo juu ya Allaah? Ametakasika Allaah juu ya hilo utakaso uliokuwa mkubwa.

Imaam Zayn-ud-Diyn al-´Iraaqiy amejibu wakati alipoulizwa kuhusu Ibn ´Arabiy:

“Kuhusiana na maneno yake kwamba Yeye ndiye yule anayeonekana na ndiye huyohuyo aliyefichikana, ni maneno yenye sumu ambayo udhahiri wake anakusudia ukomo wa vitu vyote vilivyopo kuwa ni kitu kimoja na kwamba Yeye ni mjumuiko wa viumbe Vyote. Dalili ya kuonyesha kuwa anamaanisha hivyo, ni pindi alipoweka wazi kabisa na kusema kwamba Yeye (Allaah) ni Abu Sa´iyd al-Kharraaz na vyenginevyo katika majina ya vitu vyenye kuzuka. Hivyo yule mwenye kusema hivo na mwenye kuamini hivo, ni kafiri kwa maafikiano ya wanachuoni wote.”[2]

[1] Yamenukuliwa na al-Baqaaiy´, uk. 63-64, al-Wakiyl ameyanasibisha kwa Ibn ´Arabiy katika “al-Fusuusw”, uk. 76-77.

[2] al-Baqaaiy´, uk. 66.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqiyqat-us-Suufiyyah
  • Imechapishwa: 24/12/2019