26- Muslim amepokea kupitia kwa Mu´aawiyah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa alimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Mimi ni mweka hazina tu. Yule ninayempa kwa moyo msafi basi atabarikiwa kwacho. Na yule ninayempa kwa sababu ya kuomba au kwa shari ni kama yule anayekula pasina kushiba.”[1]

27- Ameeleza pia kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiudhike kwa maombi ya ung’ang’anizi. Ninaapa kwa Allaah hakuna yeyote katika nyinyi atayeniomba na nikampa pasina kupenda kwangu na akabarikiwa kwa kile nilichompa.”[2]

28- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwua Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Masikini sio yule mwenye kupokea tonge moja ya chakula au mbili na akaenda zake au tende moja au mbili na akaenda. Masikini ni yule mwenye busara. Mkipenda someni:

لَا يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا

“Hawaombi watu kwa ung’ang’anizi.” (02:273)

29- Mng´ang´anizi ni yule mwenye kulazimisha na kufosi.

30- Sa´iyd bin al-Musayyab anaonelea yule mwenye kubaki tu msikitini ni mwombaji mng´ang´anizi. Amesema:

“Yule mwenye kubaki tu msikitini na kuwalazimisha tu wamsaidie ni aina moja wapo ya kuomba kwa kulazimisha. Anatakiwa kufanya kazi na kutafuta riziki yake.”

31- Wanachuoni wametofautiana juu ya tafsiri ya Kauli ya Allaah (Ta´aa):

لَا يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا

“Hawaombi watu kwa ung’ang’anizi.”

at-Twabariy, az-Zajjaaj na wengine wamesema:

“Hawaombi kabisa.”

Ni wenye busara na kuona haya kikamilifu. Wafasiri wengi wa Qur-aan wana maoni haya. Ni watu wenye busara na wenye kuona haya kikamilifu na hawaombi kwa kung´ang´aniza wala kwa njia nyingine yoyote.

Wengine wanasema wanaomba bila ya kung´ang´aniza. Hiki ndio chenye kufahamika wakati mtu anapoisoma Aayah. Hili linaonesha ubaya wa kuomba kwa kung´ang´aniza na kulazimisha. Kwa sababu yule mwenye kuomba kwa njia hiyo anachotaka tu ni kukusanya awe na vingi. Hivyo ndio maana watu humchukia. Upupiaji wake wa kuomba unamfanya kumpuuza Mola Wake kwa vile ameshughulishwa na kuomba watu badala ya Yule ambaye ni Mkarimu mwenye kupenda pindi watu wanapomuomba siku zote. Kinyume chake anawaomba watu wenye kuchukia wakati anapowaomba kwa kuwalazimisha Vinginevyo inajuzu kuomba wakati wa haja pasina kung´ang´aniza, kama tulivyotangulia kusema.

32- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Huenda yule ambaye nywele zake zimemchakaa na mwenye vumbi ambaye hakufunguliwa mlango akaapa kwa Allaah kupitike jambo na Allaah akamtimizia kiapo chake.”[3]

Hadiyth inatolea dalili kuonesha kuwa inajuzu kuomba midhali sio kwa kulazimisha.

[1] Muslim (1037), Ahmad (4/99) na at-Twabaraaniy (19/869).

[2] Muslim (1038), Ahmad (4/98) na an-Nasaa’iy (5/97-98).

[3] Muslim (16/174).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 18/03/2017