4- Mwanamke ambaye yuko na hedhi hahitajii kufanya Twawaaf-ul-Wadaa´. Mwanamke akikamilisha ´ibaadah za Hajj na ´Umrah kisha baadae akapatwa na hedhi kabla ya kwenda nyumbani, anaweza kwenda bila ya kufanya Twawaaf-ul-Wadaa´. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Watu waliamrishwa kufanya Twawaaf kwenye Nyumba ndio iwe kitu cha mwisho wanachofanya. Wanawake wenye hedhi tu ndio waliokhafifishiwa.”[1]

Haikupendekezwa kwa mwanamke mwenye hedhi wakati wa kuaga kwenda kwenye mlango wa msikiti Mtakatifu na kuomba du´aa. Kitu kama hicho hakikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Ibaadah zimejengwa juu ya dalili. Bali uhakika wa mambo ni kwamba kumepokelewa kinyume chake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati Swafiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alipopata hedhi baada ya Twawaaf-ul-Wadaa´ Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

“Na hebu aende.”[2]

Hakumuamrisha kwenda katika mlango wa msikiti. Lau ingelikuwa ni jambo lililowekwa katika Shari´ah basi angelibainisha.

Kuhusiana na Twawaaf ya Hajj na ´Umrah haianguki kwake. Ni wajibu kwake kuzifanya pale atapotwaharika.

[1] al-Bukhaariy (1755) na Muslim (1328).

[2] al-Bukhaariy (1762) na Muslim (1211).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016