Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah maana yake ni kumtii katika yale aliyoamrisha, kumsadikisha kwa yale aliyoeleza, kujiepusha yale aliyokataza na kuyakemea na asiabudiwe Allaah isipokuwa kwa yale Aliyoyawekea Shari´ah.

MAELEZO

Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah kuna maana na muqtadha yake. Sio matamshi yanayotamkwa peke yake. Maana yake ni kwamba unakubali kwa mdomo wako na moyo wako kwamba yeye ni Mtume wa Allaah. Unatakiwa kutamka kwa mdomo wako na uamini kwa moyo wako kwamba ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ama kutamka tu kwa mdomo wako na kupinga kwa moyo wako huo ni mwenendo wa wanafiki. Hivo ndivo alivotueleza Mtume juu yao pale aliposema:

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً

”Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah.” – na Allaah anajua vyema kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo. Wamefanya viapo vyao [vya uongo] kuwa ni kinga.”[1]

Wamefanya viapo vyao kuwa ndio kinga wanazojikinga kwazo na matokeo yake wakawa ni wenye kuzuia watu kutokamana na njia ya Allaah. Ikafahamisha kuwa kutamka kwa mdomo peke yake haitoshi.

Vivyo hivyo kuamini ndani ya moyo peke yake pasi na kutamka kwa mdomo kwa yule anayeweza kutamka haitoshi. Washirikina walikuwa wanajua kuwa yeye ni Mtume wa Allaah lakini hata hivyo wakifanya inda. Amesema (Ta´ala):

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”[2]

Wanatambua ujumbe wake ndani ya mioyo yao na wanajua kuwa yeye ni Mtume wa Allaah. Lakini kiburi na ukaidi ndio kilichowazuia kukubali ujumbe wake. Vivyo hivyo hasadi ndio iliyowazuia kama ilivyokuwa kwa mayahudi na washirikina wa kiarabu. Abu Jahl na ´Amr bin Hishaam walikuwa wakitambua hilo na wakisema kwamba wao na Banuu Haashim walikuwa wakilingana katika kila kitu lakini hata hivyo wakajigamba kuwa wako na Mtume na kwamba sisi hatuna Mtume na hatuna pa kuweza kumtoa. Matokeo yake wakapinga ujumbe wake kwa sababu ya kuwahusudu Banuu Haashim[3]. Abu Twaalib amesema katika shairi lake:

Nilijua kuwa dini ya Muhammad

ndio dini bora ya viumbe

Isingekuwa kwa ajili ya lawama na kuogopwa kutukanywa

basi ungeniona ni mwenye kufunguka waziwazi na kukubali

Alikuwa anatambua kwa moyo wake ujumbe wa Muhammad. Lakini kasumba za kipindi cha kikafiri kwa watu wake ndio zilimfanya kutokufuru dini ya ´Abdul-Muttwalib ambayo ilikuwa kuabudia masanamu. Kwa hiyo walikuwa ni wenye kutambua utume wake ndani za mioyo yao. Kwa hivyo haitoshi kutambua ndani ya moyo kuwa ni Mtume wa Allaah. Bali ni lazima mtu atamke kwa mdomo wake.

Jengine ni kwamba haitoshi kutamka kwa mdomo na kutambua ndani ya moyo. Bali ni lazima kufuatisha jambo la tatu ambalo ni kufuata. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Basi wale waliomuamini na wakamtukuza na wakamnusuru na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, hao ndio wenye kufaulu.”[4]

Haijalishi kitu hata kama mtu atamnusuru, kama mfano wa Abu Twaalib, akamuhami na akatambua kuwa ni Mtume wa Allaah lakini hata hivyo asimfuate basi mtu huyo sio muislamu mpaka amfuate. Kwa ajili hiyo ndio maana Shaykh akasema:

“Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah maana yake ni kumtii katika yale aliyoamrisha, kumsadikisha kwa yale aliyoeleza, kujiepusha yale aliyokataza na kuyakemea na asiabudiwe Allaah isipokuwa kwa yale Aliyoyawekea Shari´ah.”

Ni lazima, pamoja na kutambua ujumbe wake kwa nje, kwa ndani na kwa kuamini, kumfuata (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayo yanafupika katika nukta hizi nne zilizotajwa na Shaykh (Rahimahu Allaah):

1- Kumfuata katika yale aliyoamrisha. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume, basi kwa hakika amemtii Allaah.”[5]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Hatukutuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Allaah.”[6]

Akaambatanisha kumtii Mtume pamoja na kumtii Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) na akaambatanisha kumuasi Mtume pamoja na kumuasi Yeye:

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا

“Yeyote atakayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika atapata Moto wa Jahannam hali ya kudumu humo milele.”[7]

وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا

”Mkimtii basi mtaongoka.”[8]

وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا

”Mkimtii basi mtaongoka.”[9]

وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

”Mtiini Mtume ili mpate kurehemewa.”[10]

Kwa hiyo ni lazima kumtii yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ambaye anashuhudia ya kwamba ni Mtume wa Allaah analazimika kumtii katika yale aliyoamrisha. Hayo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.”[11]

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.”[12]

Bi maana kutokana na amri ya Mtume. Ni lazima kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

2- Kumsadikisha katika yale aliyoeleza. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza juu ya mambo mengi ya ghaibu. Ameeleza juu ya Allaah, Malaika, mambo yaliyojificha, mambo yanayokuja huko mbele katika kusimama kwa Qiyaamah, alama za Qiyaamah, Pepo, Moto, mambo yaliyopita huko nyuma na hali za nyumati zilizotangulia. Kwa hiyo ni lazima kumsadikisha katika yale aliyoelezea. Kwa sababu ni mkweli na si msema wongo. Amesema (Ta´ala):

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

”Hatamki kwa matamanio yake. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.”[13]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hazungumzi khabari hizi, maamrisho au makatazo haya chochote kutoka kichwani mwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anazungumza kutokana na Wahy kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo khabari zake ni za kweli. Asiyemsadikisha katika yale aliyoeleza sio muumini na wala hakusema kweli kwamba yeye ni Mtume wa Allaah. Ni vipi atashuhudia kuwa ni Mtume wa Allaah na amkadhibishe katika khabari zake? Ni vipi atashuhudia kuwa ni Mtume wa Allaah na asitii maamrisho yake?

3- Kujiepusha na yale aliyokataza na kugombeza. Unatakiwa kujiepusha na aliyokataza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amekukataza maneno, matendo na sifa nyingi. Hakatazi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa kwa kitu ambacho ndani yake mna madhara na shari kama ambavo haamrishi isipokuwa kwa kitu ambacho ndani yake mna kheri na wema. Mtu asipojiepusha na yale aliyomkataza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi anakuwa si mwenye kumshuhudia utume. Anakuwa ni mwenye kujigonga. Ni vipi atakuwa ni mwenye kushuhuhudia ya kwamba yeye ni Mtume wa Allaah na asijiepushe na yale aliyomkataza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.”[14]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ninapokukatazeni kitu basi jiepusheni nacho na ninapokuamrisheni jambo basi lifanyeni muwezavyo.”[15]

Ni lazima kujiepusha na aliyokataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

4- Asiabudiwe Allaah isipokuwa kwa yale aliyoweka katika Shari´ah. Jifunge katika ´ibaadah na yale ambayo Allaah amemuwekea katika Shari´ah Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa msemo mwingine usifanye ´ibaadah ambazo hazikuwekwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haijalishi kitu hata kama unataka mazuri na kheri. Lakini kitendo hichi ni batili kwa sababu hakikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nia haitoshi. Ni lazima kufuata.

´Ibaadah zinakuwa kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Haijuzu kufanya ´ibaadah ambazo hazikuwekwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[16]

“Jilazimisheni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo yaliyozuliwa. Kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[17]

Kufanya matendo ambayo hayakuwekwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunazingatiwa ni Bid´ah yenye kukemewa na iliyokatazwa. Haijalishi kitu hata kama fulani anaonelea hivo au imefanywa na mtu fulani. Midhali imetoka nje ya yale aliyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni Bid´ah na upotevu. Haabudiwi Allaah isipokuwa kwa yale aliyoweka kupitia kwa Mtume Wake. Mambo yaliyozuliwa na mambo ya ukhurafi yote ni batili na upungufu kutoka kwa yule mwenye kuyafanya. Haijalishi kitu hata kama anakusudia kheri na anataka ujira. Kinachozingatiwa sio makusudio. Kinachozingatiwa ni ufuataji, kutii na kunyenyekea. Tungelikuwa huru kufanya tuyatakayo na kukithirisha ´ibaadah tuzikatazo basi tusingelikuwa na haja ya kutumiliziwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hiyo ni katika rehema ya Allaah kwetu kwamba hakututegemeza juu ya akili yetu wala hakututegemeza kwa mtu fulani. Kwa sababu mambo haya mategemezi yake ni katika Shari´ah na kwa Allaah Wake. Hakuna kinachonufaisha isipokuwa kile chenye kuafikiana na Shari´ah Yake na Mtume Wake.

Katika haya kuna kujitenga mbali na Bid´ah zote. Yule mwenye kuzusha kitu katika dini ambacho hakikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakushuhudia ya kwamba yeye ni Mtume wa Allaah. Hakushuhudia shahaadah ya kweli. Kwa sababu yule ambaye anashuhudia kuwa ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) shahaadah ya kikweli anajifunga na yale aliyoyaweka katika Shari´ah na wala hazushi kitu kutoka kichwani mwake au akafanya kitu kilichozuliwa na ambaye kamtangulia. Hii ndio maana ya kushuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah. Sio matamshi yanayotamkwa mdomoni pasi na kulazimiana, kuyatendea kazi na mtu kujifungamanisha na yale yaliyokuja na Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 63:01-02

[2] 06:33

[3] Tazama ”Siyrat-un-Nabawiyyah” (01/251) ya Ibn Hishaam.

[4] 07:157

[5] 04:80

[6] 04:64

[7] 72:23

[8] 24:54

[9] 24:54

[10] 24:56

[11] 59:07

[12] 24:63

[13] 53:03-04

[14] 59:07

[15] al-Bukhaariy (7688) na Muslim (1337).

[16] al-Bukhaariy (7350) hali ya kuiwekea taaliki na Muslim (18) (1718).

[17] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676), Ibn Maajah (42, 43), Ahmad (28/373) (17144).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 180-186
  • Imechapishwa: 18/01/2021