89. Dalili juu ya kwamba imani ni maneno, kuamini na vitendo na kwamba inazidi na kupungua


Miongoni mwa mambo yanayofahamisha kuwa imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini kwa moyo na matendo ya viungo ni ile Hadiyth iliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo amesema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu. Ya juu yake kabisa ni “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” na ya chini yake ni kuondosha chenye kuudhi njiani na kuwa na hayaa ni tanzu katika imani.”[1]

Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah ni kutamka kwa ulimi.

Kuwa na hayaa ni tanzu katika imani ni kitendo cha moyo.

Kuondosha chenye kuudhi njiani ni kitendo cha viungo.

Ni dalili inayofahamisha kuwa imani ni maneno, kuamini na matendo.

Kitendo cha kwamba inazidi kwa utiifu ni jambo limetajwa wazi katika Qur-aan:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا

“Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea. [Hao ni wale] ambao wanasimamisha swalah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa – hao ndio waumini wa kweli!  Wana daraja kwa Mola wao na maghfirah na riziki karimu.” (08:02-04)

Amefanya swalah na kujitolea ni katika imani. Hivi ni vitendo vya viungo. Kumdhukuru Allaah ni maneno ya ulimi. Maneno Yake:

زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

“… huwazidishia imani… ”

ni dalili yenye kuonesha kuwa imani inazidi. Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا

“Inapoteremshwa Suurah, basi miongoni mwao wako wanaosema: “Nani kati yenu [Suurah] hii imemzidishia imani?” Ama wale walioamini huwazidishia imani nao wanafurahia.”” (09:124)

وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا

“Na iwazidishie imani wale walioamini.” (74:31)

Ni dalili zinazofahamisha kuwa imani inazidi kwa kufanya utiifu. Kadhalika imani inashuka kwa kufanya maasi kutokana na dalili ya Hadiyth inayosema:

“Ambaye ataona maovu katika nyinyi ayaondoshe kwa mkono wake, asipoweza afanye hivo kwa ulimi wake, asipoweza afanye hivo kwa moyo wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”

Ni dalili yenye kuonesha kuwa imani inakuwa dhaifu. Ambaye hakemei maovu si kwa mkono wala ulimi wake ana imani dhaifu. Na yule asiyekemea si kwa mkono wake, ulimi wake wala moyo wake hana imani kabisa kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nyuma na hilo hakuna imani yoyote sawa na mbegu ya hardali.”

Vilevile imekuja katika Hadiyth ya kwamba:

“Allaah atamtoa Motoni yule ambaye ndani ya moyo wake mna imani ndogo ndogo ndogo kabisa sawa na mbegu ya hardali.”

Hii ni dalili inayoonesha kuwa imani inadhoofika kiasi cha kwamba inakuwa sawa na uzani wa mbegu ya hardali au chini ya hapo. Vilevile amesema (Ta´ala):

هُمْ لِلْكُفْرِ يَوْمَئِذٍ أَقْرَبُ مِنْهُمْ لِلْإِيمَانِ

“Wao siku ile walikuwa karibu na ukafiri kuliko imani.” (03:167)

Ni dalili inayoonesha kuwa imani inakuwa dhaifu mpaka inamfanya mwenye nayo kukaribia ukafiri:

هُمْ لِلْكُفْرِ يَوْمَئِذٍ أَقْرَبُ مِنْهُمْ لِلْإِيمَانِ

“Wao siku ile walikuwa karibu na ukafiri kuliko imani.”

Hii ni dalili ya upunguaji wa imani.

[1] al-Bukhaariy (09) na Muslim (35) na (57)