88. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya imani na Radd kwa wanaoonelea kinyume

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

وقلْ إنمَا الإِيمانُ قولٌ ونِيةٌ

36 – Sema kuwa imani ni maneno na nia

وفعلٌ عَلَى قولِ النبِي مُصَرحُ

     na kitendo kutokana na [ushahidi wa] maneno ya Mtume yaliyo wazi

Hii ni ´Aqiydah ya tatu. Anachomaanisha ni kwamba achana na ´Aqiydah ya Khawaarij na achana vilevile na ´Aqiydah ya Murji-ah na badala yake shikamana na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ya kwamba: imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini kwa moyo na matendo ya viungo na kwamba inazidi kwa kufanya utiifu na inapungua kwa kufanya maasi. Hii ndio maana kamilifu iliyochukuliwa kutoka kwenye dalili. Haikuchukuliwa kutoka katika matamanio na fikira. Imani inapatikana kwa kuwepo mambo manne:

1 – Kutamka kwa ulimi.

2 – Kuamini kwa moyo.

3 – Matendo ya viungo.

4 – Inazidi kwa utiifu na inapungua kwa maasi.

Imani sio [kuamini] kwa moyo peke yake, kama wanavyoamini Ashaa´irah.

Imani sio kuamini kwa moyo na kutamka kwa ulimi peke yake, kama wanavyoamini Ahnaaf.

Imani sio kutamka kwa ulimi peke yake, kama wanavyoamini Karraamiyyah.

Imani sio kutambua ndani ya moyo, kama wanavyoamini Jahmiyyah. ´Aqiydah yao chafu inapelekea juu ya kwamba Fir´awn ni muumini. Kwa sababu alitambua kwa moyo wake [ukweli wa] yale aliyokuja nayo Muusa (´alayhis-Salaam):

قَالَ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا أَنزَلَ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ

“Hakika umekwishajua kwamba hakuna aliyeteremsha haya isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi.” (17:102)

Alikuwa akiyatambua haya kwa moyo wake. Lakini hata hivyo aliyakana kwa sababu ya kiburi tu na ili aweze kubaki juu ya ufalme wake. Hivyo ndio maana akawa ameyafanyia ujeuri yale aliyokuja nayo Muusa (´alayhis-Salaam).

Vilevile washirikina wanatambua kwa mioyo yao ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah na kwamba yuko juu ya haki. Amesema (Ta´ala):

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Kwa hakika Tunajua kuwa yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe, lakini madhalimu wanakanusha Aayah za Allaah.” (06:33)

Wao si kwamba wanamkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kilichofanya kumkhalifu ni ukanushaji, kiburi, kuwa na jeuri juu ya haki na kasumba juu ya batili. Hayahaya ndiyo yalifanywa Abu Twaalib, ambaye ni ami yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alitambua kuwa Mtume ndiye yuko katika haki. Amesema:

Hakika nimejua kuwa dini ya Muhammad

ndio dini bora kabisa ya viumbe

Pindi alipokuwa si mwenye kumfuata na akafa juu ya dini ya ´Abdul-Muttwalib – ambayo ilikuwa juu ya shirki – akawa ni katika watu wa Motoni. Pamoja na kwamba alikuwa akitambua kuwa dini ya Muhammad ni haki. Amesema:

Lau si lamawa au kuchelea kutukanwa

basi mgeniona kwa hayo ni mwenye kujisalimisha waziwazi

Hakuna kilichomzuia kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa kuwa na mori juu ya dini za mababa na mababu zake. Mori ndio ukamzuia na matokeo yake akafa juu ya ukafiri. Vinginevyo anajua kuwa Muhammad yuko katika haki na anaamini hili. Kwa mujibu wa ´Aqiydah ya Ashaa´irah inapelekea kwamba ni muumini.

Imani sio kutamka kwa ulimi peke yake bila ya kuamini ndani ya moyo kama, wanavyoamini Karraamiyyah. Kwa mujibu wa ´Aqiydah hii wanafiki watakuwa ni waumini. Wanatambua kwa ndimi zao lakini hata hivyo wanapinga kwa mioyo yao. Pamoja na hivyo Allaah amewahukumu kwamba wako katika tabaka ya chini kabisa Motoni chini ya washirikina. Amesema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ

“Miongoni mwa watu wako wanaosema… “

Bi maana wanatamka.

آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ

“Tumemuamini Allaah na siku ya Mwisho hali ya kuwa si wenye kuamini.” (02:08)

Bi maana wanatamka kwa ndimi zao. Katika Aayah nyingine anasema:

يَقُولُونَ بِأَفْوَاهِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ

“Wanasema kwa midomo yao yale yasiyokuwemo katika nyoyo zao.” (03:167)

Kutamka kwa ulimi peke yake haitoshi. Bali Allaah amesema juu yao:

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah” na Allaah anajua fika kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo. Wamefanya viapo vyao kuwa ni kinga… “

Bi maana sitara.

فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا فَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ

“… hivyo wakazuia [watu na] njia ya Allaah, hakika ni uovu mbaya mno waliokuwa wakitenda. Hayo ni kwa kuwa wao waliamini, kisha wakakufuru.” (63:01-02)

Wamesema kuwa wameamini kwa ndimi zao kisha wakakufuru kwa nyoyo zao. Kutamka kwa ulimi peke yake haitoshi hata kama mtu atatambua kwa ulimi. Sivyo tu, hata kama mtu atapigana vita na akapambana bega kwa bega akiwa pamoja na waislamu. Haitoshi hata kama ataswali na kufunga mpaka aamini kwa moyo wake yale yaliyotamkwa na ulimi wake.

Vilevile imani sio kutamka kwa ulimi na kuamini kwa moyo, kama wanavyoamini Fuqahaa´ wa Murji-ah. Mambo yangalikuwa hivyo basi maamrisho na makatazo visingelikuwa na faida yoyote. Ingelitosha kwa mtu kuamini kwa moyo wake na kutamka kwa ulimi wake hata kama hatoswali, hatofunga n.k. Ni jambo halina shaka kuwa haya ni ´Aqiydah batili. Ni ´Aqiydah inatokomeza matendo yote. Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika Aayah nyingi ameambatanisha matendo pamoja na imani:

آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ

“Wameamini na wakatenda mema.” (11:23)

Hakusema wale walioamini peke yake au wale waliotenda matendo mema peke yake. Ni lazima yapatikane yote mawili kwa pamoja. Matendo peke yake pasi na imani hayatoshi na wala imani peke yake pasi na matendo haitoshi. Ni lazima kupatikane imani na matendo mema vyote viwili. Haya ndio yaliyokuja katika Aayah nyingi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 186-189
  • Imechapishwa: 13/01/2024