Sharti zake ni saba. Haimnufaishi mtu isipokuwa kwa sharti hizi saba:

1- Elimu ambayo kinyume chake ni ujinga. Anayesema “hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah” na wakati huohuo hajui maana yake, basi huyu haitomfaa kitu shahaadah.

2- Yakini ambayo kinyume chake ni mashaka. Baadhi ya watu wanaweza kuwa wanajua maana yake lakini hata hivyo wako na shaka juu ya hilo. Elimu yake si kweli. Ni lazima mtu awe na yakini ya ´hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah` na kwamba ni haki.

3- Ikhlaasw ambayo kinyume chake ni shirki. Baadhi ya watu wanasema “hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah” lakini pamoja na hivyo hawaachi shirki. Ni kama hali ilivyo hii leo kwa waabudia makaburi. Watu hawa haitowafaa kitu shahaadah kwa sababu miongoni mwa sharti zake ni kuacha shirki.

4- Ukweli ambao kinyume chake ni uongo. Kwa sababu wanafiki walikuwa wakisema “hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah” lakini hata hivyo ni waongo ndani ya mioyo yao. Hawaamini maana yake. Amesema (Ta´ala):

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً

”Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah.” – na Allaah anajua vyema kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo. Wamefanya viapo vyao [vya uongo] kuwa ni kinga.”[1]

5- Mapenzi. Mtu anatakiwa kulipenda neno hili na kuwapenda wenye nalo. Kuhusu yule ambaye halipendi au hawapendi wenye nalo haliwezi kumnufaisha.

6- Kunyenyekea ambako kinyume chake ni kuacha. Mtu anapaswa kunyenyekea yale yanayofahamishwa nalo katika kumwabudu Allaah Mmoja hali ya kuwa yupekee hana mshirika na kutekeleza maamrisho yake. Maadamu umekubali na umesuhudia ya kwamba  hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah basi inakulazimu kunyenyekea hukumu na dini Yake. Ama kusema “hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah” pasi na kunyenyekea hukumu za Allaah na Shari´ah Yake basi haitokufaa kitu shahaadah.

7- Kukubali ambako kinyume chake ni kurudisha. Kwa msemo mwingine ni kwamba hutakiwi kurudisha nyuma kitu chochote katika haki za shahaadah na yale yanayofahamishwa nalo. Unatakiwa kuikubali kikweli.

 Wako waliozidisha sharti ya nane ambayo ni kujitenga mbali na shirki. Mtu hawi mpwekeshaji mpaka ajitenge mbali na shirki:

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاء مِّمَّا تَعْبُدُونَ  إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ

”Ibraahiym alipomwambia baba yake na watu wake: “Hakika mimi najitoa dhima na yale yote mnayoyaabudu [ya batili]! [Simwabudu mwengine yeyote] isipokuwa Yule ameniumba, basi hakika Yeye ataniongoa.”[2]

Hizi ndio sharti za shahaadah. Ni sharti nane.

[1] 63:01-02

[2] 43:26

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 173-174
  • Imechapishwa: 11/01/2021