86- Wala haijuzu kuliswalia jeneza ndani ya nyakati tatu ambazo imeharamishwa kuswali ndani yake isipokuwa kwa dharurah. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anatukataza kuswali au kuwazika maiti zetu ndani ya nyakati tatu; mpaka lichomoze jua kwa kutoa miale yake hadi liinuke, pale linaposimama katikati ya utosi mpaka jua lipinduke na wakati jua linamili kuelekea kuzama mpaka lizame.”

Ameipokea Muslim (02/208), Abu ´Awaanah katika “as-Swahiyh” yake (01/386), Abu Daawuud (02/66), an-Nasaa´iy (01/277), at-Tirmidhiy (02/144) ambaye ameisahihisha. Vilevile al-Bayhaqiy (04/32), at-Twayaalisiy (nambari. 1001) na Ahmad (04/152) kupitia kwa ´Ulayy bin Rabaah ambaye amepokea kutoka kwake. al-Bayhaqiy amezidisha:

“Amesema: “Nilisema kumwambia ´Uqbah: “Kunazikwa usiku?” Akasema: “Ndio. Abu Bakr alizikwa usiku.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.

Hadiyth, kwa kuenea kwake, inahusu pia swalah ya jeneza. Ndio jambo lililofahamika kwa Maswahabah. Maalik amepokea katika “al-Muwattwa” (01/228) al-Bayhaqiy amepokea kupitia njia yake, kutoka kwa Muhammad bin Harmalah kwamba Zaynab msichana wa Abu Salamah alikufa na kipindi hicho Twaariq ndiye alikuwa mkuu wa al-Madiynah. Jeneza lake likaletwa baada ya Fajr ambapo likawekwa al-Baqiy´. Twaariq alikuwa akiswali Fajr wakati kunaanza kung´aang´aa. Ibn Abiy Harmalah amesema: “Nimemsikia ´Abdullaah bin ´Umar akisema kuwaambia jamaa zake:

“Ima mumswalie sasa hivi au mumwache mpaka jua liinuke.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.

Kisha Maalik akapokea kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye amesema:

“Jeneza liswaliwe baada ya ´Aswr na baada ya Fajr zitaposwaliwa ndani ya wakati wake.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh pia.

al-Bayhaqiy amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri kutoka kwa Ibn Jurayj, Ziyaad amenieleza kwamba ´Aliy amempa khabari kuwa kuna jeneza moja liliwekwa katika makaburi ya watu wa Baswrah pindi jua lilikuwa manjanomanjano. Jeneza lile halikuswaliwa mpaka jua lilipozama. Abu Barzah akaamrisha mwenye kunadi anadi swalah kisha akakimu. Abu Barzah akatangulia mbele akawaswalisha Maghrib na kati yetu alikuweko Anas bin Maalik. Abu Barzah ni katika Answaar wa Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kisha wakaliswalia jeneza.

al-Khattwaabiy amesema katika “al-Ma´aalim” (04/327) ambayo ufupizo wake ni ifuatavyo:

“Watu wametofautiana juu ya kufaa kumswalia maiti na kumzika ndani ya nyakati hizi tatu. Wanachuoni wengi wakaonelea kwamba imechukizwa kumswalia ndani ya nyakati hizi tatu. Haya ndio maoni ya ´Atwaa´, an-Nakha´iy, al-Awzaa´iy, ath-Thawriy, watu wa rai, Ahmad na Ishaaq. ash-Shaafi´iy anaona kuwa inafaa kuswali na kuzika wakati wowote wa usiku au mchana. Maoni ya wanachuoni wengi ndio yenye haki zaidi kwa sababu ya kuafikiana kwake na Hadiyth.”

Kutokana na hayo utajua kwamba madai ya an-Nawawiy kujuzisha swalah hii kwa maafikiano ni kosa na usahaulifu kutoka kwake (Rahimahu Allaah).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 165-166
  • Imechapishwa: 08/02/2022