86. Tofauti ya Ahl-us-Sunnah na Ahl-ul-Bid´ah katika kukabiliana na Sunnah

Hakuna tofauti, kama tulivyosema, kati ya Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vyote viwili vinatoka kwa Allaah. Ahl-ul-Dhwalaal ndio wanatofautisha kati ya Qur-aan na Sunnah. Wao ndio ambao wanasema kwamba hawakubali isipokuwa Qur-aan pekee. Hoja yao ni kwamba eti Qur-aan haiwezi kuingiliwa na shaka yoyote tofauti na Sunnah. Wanaona kuwa Sunnah inaweza kuingiwa na mashaka kwa mtazamo wao. Ama kwa mtazamo wa waislamu haingiliwi na mashaka. Kwa kuwa ni katika mapokezi ya waaminifu na wenye kuhifadhi ambao wameyanukuu kwa amana. Wao hawazitilii shaka yoyote Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba ni yenye kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Ama kuhusu wanafiki au wale ambao ndani ya nyoyo zao kuna upungufu wa imani kama vile Khawaarij, Mu´tazilah na mapote mengine yana mashaka. Baadhi yao wanatilia mashaka Sunnah yote na wala hawaoni kuwa ina nafasi yoyote na wanasema kwamba wametoshelezwa na Qur-aan. Baadhi yao wanatilia mashaka baadhi ya Sunnah na wanasema kwamba wao wanakubali tu yale mapokezi yaliyopokelewa kupitia njia nyingi na wanarudisha mapokezi yaliyopokelewa kwa njia moja na wanasema kuwa hayafidishi zaidi ya dhana tu. Lakini Ahl-ul-Haqq wanaonelea, yale yote yaliyosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni mamoja yakiwa yamepokelewa kwa njia nyingi au kwa njia moja, kwa hakika yanafidisha elimu na yakini na wanayatumia kama hoja na dalili katika mambo ya ´Aqiydah, ´ibaadah na mu´amala. Hawayatilii mashaka. Upande mwingine Ahl-ul-Dhwalaal wanasema kuwa mapokezi yaliyopokelewa kwa njia moja hayatumiwi kama hoja katika mambo ya ´Aqiydah kwa sababu wanaona yanafidisha dhana na kwamba eti ´Aqiydah inajengwa juu ya yakini.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 114-115
  • Imechapishwa: 27/11/2018