Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah amewafaradhishia viumbe vyote kukanusha Twaaghuut na badala yake kumuamini Allaah. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Twaaghuut ni kila chenye kuabudiwa, kinachofuatwa au kutiiwa ambacho mja anapindukia mipaka yake.”

MAELEZO

Hapa Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) anataka kuonyesha kuwa Tawhiyd haiwezi kutimia isipokuwa kwa kumwabudu Allaah pekee hali ya kuwa hana mshirika na kujitenga mbali na shirki. Allaah amefaradhisha hayo juu ya waja Wake.

Twaaghuut msingi wake umetokana na neno “Twughyaan” na maana yake ni “kupindukia mipaka”. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا لَمَّا طَغَى الْمَاءُ حَمَلْنَاكُمْ فِي الْجَارِيَةِ

”Maji yalipofurika, hakika Sisi tulikubebeni katika chombo kinachokwenda.” (al-Haaqqah 69 : 11)

Bi maana wakati maji yalipozidi juu ya kipimo chake cha kawaida, Tulikubebeni juu ya chombo kinchotembea ambacho ni safina.

Kuhusu maana yake ya Kishari´ah bora zaidi ni yale yaliyosemwa na Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah):

“Twaaghuut ni kila chenye kuabudiwa, kinachofuatwa au kutiiwa ambacho mja anapindukia mipaka yake.”

Hata hivyo hawa wenye kuabudiwa, wanaofuatwa na kutiiwa hawahusiani na wale waja wema. Waja wema hawazingatiwi kuwa ni Twaaghuut ijapokuwa wataabudiwa, watafutwa au kutiiwa. Masanamu yanayoabudiwa badala ya Allaah ni Twaaghuut. Kadhalika wanazuoni waovu wanaolingania katika upotevu, kufuru, Bid´ah, kuhalalisha aliyoharamisha Allaah na kuharamisha aliyohalalisha Allaah. Wao pia ni Twaaghuut. Wale wanaowapendezeshea watawala ili kuacha kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah na badala yake kuchukua zile sheria zilizotungwa watu pia wao ni Twaaghuut. Watu hawa wamepindukia mipaka yao. Mpaka wa mwanachuoni ni yeye kufuata yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu mwanachuoni wa kihakika ni mrithi wa Mitume. Wanarithi elimu yao, matendo yao, tabia, Da´wah na kuwafundisha Ummah wao. Wakivuka mpaka huu na wakaanza kuwapambia watawala kuacha kuhukumu kwa Shari´ah ya Kiislamu, basi wanazingatiwa kuwa ni Twaaghuut. Hili linatokana na kwamba wamevuka mipaka ambayo ni wajibu kwao kufuata.

Kuhusiana na maneno yake “kutiiwa”, anachomaanisha ni wale watawala ambao wanatiiwa utiifu wa Kishari´ah au utiifu wa kilimwengu. Watawala wanatiiwa utiifu wa Kishari´ah pale ambapo wanaamrisha kitu kisichoenda kinyume na maamrisho ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika hali hii si sawa kuwachukulia kuwa ni Twaaghuut. Badala yake ni wajibu kwa raia kusikiliza na kutii. Watawala kutiiwa katika hali kama hii na kwa kidhibiti hichi ina maana ya kumtii Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hiyo inatakiwa kwetu kumwabudu Allaah (Ta´ala) na kujikurubisha Kwake pindi tunapomtii mtawala katika yale ambayo ni wajibu kumtii. Ni wajibu kwetu kufanya hivo kwa sababu Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ
“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.” (an-Nisaa´ 04 : 59)
Ama kuhusu kuwatii watawala utiifu wa kilimwengu, watu wawatii ikiwa wana nguvu katika utawala wao kwa sababu wana nguvu na sio kwa sababu ya imani. Mtawala anatakiwa kutiiwa kwa ajili ya imani. Aina ya utiifu huu ndio yenye manufaa. Inawanufaisha watawala wenyewe na inawanufaisha raia pia. Vilevile wanaweza kutiiwa kwa sababu wananchi wanakhofia nguvu za mtawala.

Kwa ajili hiyo hali za raia na watawala zimegawanyika aina mbalimbali:

1- Utiifu kwa mtawala unaotokamana na imani na utawala wenye nguvu. Hii ndio aina iliyo juu kabisa.

2- Utiifu kwa mtawala unaotokamana na imani na utawala dhaifu. Hii ndio aina ya chini kabisa na aina ya khatari zaidi, sawa kwa jamii, mtawala na wananchi. Ikiwa kizuizi cha imani na vizuizi vya utawala ni dhaifu, basi kunatokea ghasia katika mawazo, tabia na matendo.

3- Kule kutiiwa kwa mtawala kwa sababu ya imani kunakuwa dhaifu na kunakuwa na nguvu kwa sababu ya utawala. Aina hii iko kati na kati. Itakuwa ni bora kwa jamii ikiwa watamtii mtawala kwa sababu ya utawala wake. Ikiwa kinga hii pia itadhoofika, basi usiulize hali ya unyonge itayokuwa nayo jamii na matendo yake maovu.

4- Kule kutiiwa kwa mtawala kwa sababu ya imani kunakuwa na nguvu na kunakuwa ni dhaifu kwa sababu ya utawala. Katika hali hii muonekano wa jamii hautoonekana mzuri kama ulivo ule wa tatu. Hata hivyo mafungamano kati ya watu na Mola Wao yanakuwa ni kamilifu na ni yenye nguvu zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 150-152
  • Imechapishwa: 04/06/2020