86. Allaah atakuja siku ya Qiyaamah

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atakuja siku ya Qiyaamah na Malaika wakiwa safusafu kwa ajili ya kufanyia hesabu Ummah, kuwaadhibu na kuwalipa.

MAELEZO

Miongoni mwa mambo yatayokuwa siku ya Qiyaamah ambayo ni lazima kuyaamini ni kwamba Allaah atakuja kuhukumu kati ya waja Wake. Atakuja. Amesema (Ta´ala):

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ

“Je, wanangojea nini isipokuwa Allaah awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika?”[1]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) na Malaika watakuja. Malaika watakuja wakiwa safusafu na kuwazunguka viumbe katika uwanja wa Mkusanyiko. Atakuja kuwahukumu waja Wake kwa njia inayolingana na utukufu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Haya yameelezwa Naye na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuja kwa Allaah (´Azza wa Jall) ni sifa ya kimatendo. Atakuja vipi? Hatujui. Hatuna utambuzi juu ya namna, lakini atakuja vile anavotaka. Lakini hata hivyo tunaamini ujio Wake. Ni jambo linaingia ndani ya ´Aqiydah. Kuhusu wale wanaopindisha maana ya ujio kwamba ni kuja kwa amri Yake ni upindishaji batili. Allaah ndiye ambaye amesema kuwa atakuja, hakusema amri Yake ndio itakuja. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye atakuja kwa dhati Yake ujio ambao unalingana na utukufu Wake.

[1] 2:210

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 64
  • Imechapishwa: 19/08/2021