Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Ameumba Moto na akaufanya kuwa ni makazi ya wale wenye kumkufuru na akazikanusha Aayah, Vitabu na Mitume Yake. Amewafanya ni wenye kuzuiwa kutokamana na kumuona.

MAELEZO

Kuamini siku ya Qiyaamah kumekusanya yale yote yatayopitika ndani ya siku hiyo – kila ambacho Allaah amekitaja ndani ya Kitabu Chake au Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Sunnah yake. Ni lazima kwetu kuamini kila kitachotokea siku ya Qiyaamah. Tunaamini kuwa Allaah ameumba Pepo na akawaandalia nayo waja Wake wachaji na waumini. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ

“Wape bishara njema wale walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo chini yake mito.”[1]

Pepo ni makazi ya waumini siku ya Qiyaamah. Ni makazi ya milele na yasiyokwisha; katu hawatotolewa ndani yake, hawatokufa, hawatopatwa na magonjwa, kuzeeka wala kupatwa na kitu cha kuchukiza. Ni neema za milele na zenye kuendelea.

Miongoni mwa mambo yatayokuwa siku ya Qiyaamah ni Moto. Allaah ameuumba na akawaandalia makafiri. Amesema (Ta´ala):

فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا وَلَن تَفْعَلُوا فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ

“Msipofanya, na wala hamtoweza kufanya, basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe.”[2]

Pepo na Moto vyote viwili vimekwishaumbwa hivi sasa kwa sababu Allaah anasema:

أُعِدَّتْ

“… imeandaliwa… ”[3]

Haina maana kwamba vitaumbwa siku ya Qiyaamah. Vyote viwili vimekwishaandaliwa; Pepo imeadandaliwa kwa ajili ya wenye kumcha Allaah na Moto umeandaliwa kwa ajili ya makafiri. Miongoni mwa mambo yanayojulisha kuwa Moto umekwishaumbwa ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Moto ulilalamika kwa Mola ukasema: “Ee Mola! Nalika kwa ndani.” Akaupa idhini ya kupumua mara mbili; pumzi ya kwanza wakati wa masika na pumzi ya pili wakati wa kipwa. Ndio lile joto kali mnalohisi na baridi kali mnayohisi.”[4]

Ni dalili inayojulisha kwamba vipo na vimeandaliwa hivi sasa.

Kuamini Pepo na Moto ni jambo linaloingia katika imani ya kuamini siku ya Qiyaamah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye ataamini ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah na kwamba ´Iysaa ni mja na Mtume Wake na ni neno alilolirusha kwa Maryam na roho inayotokamana Naye na kwamba Pepo ni haki na Moto ni haki, basi Allaah atamwingiza Peponi pasi na kujali yale matendo aliyofanya.”[5]

Kwa hivyo ni lazima kuamini Pepo na Moto. Haitoshi kuamini Pepo na Moto, bali ni lazima vilevile kufanya matendo ambayo yatakuwezesha kuingia Peponi na uyaepuke matendo yanayokusababishia kuingia Motoni.

[1] 2:25

[2] 2:24

[3] 3:133

[4] al-Bukhaariy (537).

[5] al-Bukhaariy (3435) na Muslim (28).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 63-64
  • Imechapishwa: 19/08/2021