85. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya mtenda dhambi


Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wao wako juu ya haki na uadilifu. Hawamkufurishi mtenda dhambi kubwa na wala hawasemi kuwa ana imani kamilifu. Wanasema kuwa ni muumini mwenye imani pungufu au kwamba ni muumini mtenda dhambi kubwa. Ni muumini kwa imani yake na ni mtenda dhambi kwa dhambi yake kubwa aloitenda. Mtu kama huyu yuko chini ya matakwa kwa njia ya kwamba Allaah akitaka atamsamehe na akitaka pia atamuadhibu. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.” (04:48)

 Ikibidi kuadhibiwa hatodumishwa Motoni milele kama wanavyoonelea Khawaarij na Mu´tazilah.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameoanisha baina ya Aayah za ahadi na za matishio. Hawasemi kuwa maasi hayadhuru kitu, kama wanavyosema Murji-ah, na wala hawasemi kuwa yanakufurisha, kama wanavyosema Khawaarij. Bali wanasema kuwa maasi yanadhuru na kuipunguza imani. Lakini hata hivyo hayamtoi mwenye nayo katika dini. Wameyaoanisha maandiko. Haya ndio madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuhusu mtenda dhambi kubwa. Hii ndio maana ya maneno ya mwandishi (Rahimahu Allaah):

Usiwakufurishe wenye kuswali hata kama watatenda maasi

Bi maana watu wa Qiblah kati ya waumini na waislamu.

hata kama watatenda maasi… – Bi maana maadamu maasi yao yako chini ya kufuru na shirki.

wote wanatenda dhambi – Hakuna yeyote aliyesalimika na maasi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nyote ni wenye kukosea sana. Wabora wa wenye kukosea ni wale wenye kutubia.”[1]

Mwenye ´Arshi anasamehe – Bi maana anaghufiri. Amesema (Ta´ala):

وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“… na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.”

Katika Hadiyth ya kiungu imekuja:

“Lau utanijia na ardhi nzima imejaa makosa kisha ukakutana na Mimi na hukunishirikisha na chochote nitakujia na msamaha kiasi hicho.”[2]

Ikiwa mtu ni katika watu wenye kumuabudu Allaah peke yake na hakufanya shirki, bali ana madhambi yaliyo chini ya shirki, mtu kama huyu kuna matumaini juu yake kupata msamaha wa Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

“Sema: “Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: “Msikate tamaa na huruma wa Allaah, hakika Allaah anasamehe dhambi zote, hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.”” (39:53)

Anaweza kuwasamehe kama ambavyo vilevile anaweza akawaadhibu kwa madhambi yao. Lakini ikibidi kuwaadhibu hatowadumisha Motoni milele.

Haya ndio madhehebu yaliyo kati na kati baina ya kupetuka mipaka na kuzembea juu ya watenda madhambi.

[1] at-Tirmidhiy (2499), Ibn Maajah (4251), Ahmad (03/198) na wengineo

[2] Ahmad (05/147) na al-Haakim (04/241)