84. Mtazamo wa Khawaarij, Mu´tazilah na Murji-ah juu ya mtenda dhambi

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

ولاَ تُكْفِرنْ أَهلَ الصلاةِ وإِنْ عَصَوْا

33 – Usiwakufurishe wenye kuswali hata kama watatenda maasi

فَكُلهُمُ يَعْصِي وذُو العَرشِ يَصفَحُ

     wote wanatenda dhambi na Mwenye ´Arshi anasamehe

MAELEZO

Haya ni masuala kuhusu kuwakufurisha watenda madhambi makubwa yaliyo chini ya shirki. Kumetokea tofauti kubwa kati ya Khawaarij, Mu´tazilah na Murji-ah na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Khawaarij wanakufurisha kwa kutenda dhambi kubwa ilio chini ya shirki na wanaonelea kuwa wenye nayo watadumishwa Motoni milele. Kadhalika wanahalalisha kumwaga damu na kuchukuliwa mali zao kwa kujengea kwamba ni makafiri. Wanajengea hoja kwa Aayah zilizothibiti zinazokemea juu ya madhambi na maasi na wanazifasiri kwamba zinamkufurisha mwenye madhambi hayo.

Mu´tazilah wanasema kuwa sio kafiri wala muumini. Bali yuko katika daraja ilio kati ya daraja mbili.

Kuhusu Murji-ah wanatofautiana nao. Hawaonelei kuwa dhambi kubwa inaidhuru kitu imani wala kuipunguza. Mtenda dhambi kubwa kwa mujibu wao ni muumini mwenye imani kamilifu. Wanaona kuwa imani haidhuriki kitu ikiambatana na madhambi kama ambavyo utiifu haunufaishi kitu ukiambatana na ukafiri. Hii ndio ´Aqiydah ya Murji-ah kwa kifupi. Kwa sababu hawayaingizi matendo ndani ya imani. Wanaona kuwa mwenye kuacha jambo la wajibu, akafanya jambo la haramu au akafanya dhambi kubwa ilio chini ya shirki ni mwenye imani kamilifu na haipungui kwa maasi kama ambavyo haiongezeki kwa utiifu. Kwa mujibu wao imani ni kitu kimoja kisichozidi na kisichopungua. Hii ndio ´Aqiydah ya Murji-ah inayopingana na ´Aqiydah ya Khawaarij. Murji-ah wamechukua Aayah za ahadi na matarajio na wakaacha Aayah za matishio na makemeo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 180-181
  • Imechapishwa: 13/01/2024