83- Kisha atoe Tasliym mbili kama anavofanya katika swalah ya faradhi; moja upande wa kuumeni mwake na nyingine upande wa kushotoni mwake. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Mambo matatu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiyafanya ambayo watu wameyaacha; moja yao ni kutoa Tasliym katika jeneza mfano wa Tasliym katika swalah.”

Ameipokea al-Bayhaqiy (04/43) kwa cheni nzuri. an-Nawawiy amesema (05/239):

“Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.”

Katika “Majma´-uz-Zawaa-id” (03/34) imekuja:

“Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” na wapokezi wake ni waaminifu.”

Imethibiti katika “Swahiyh-ul-Muslim” na kwenginepo kupitia kwa Ibn Mas´uud kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoa Tasliym mbili ndani ya swalah.

Hili linabainisha kwamba makusudio ya maneno yake katika Hadiyth ya kwanza:

“Mfano wa Tasliym katika swalah.”

kwamba ni zile Tasliym mbili zilizozoeleka.

Upo uwezekano pia kuwa alikuwa amekusudia kwa kuongezea hilo kwamba alikuwa akitoa Tasliym moja vilevile kwa kuzingatia kwamba hilo pia ilikuwa ni miongoni mwa Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika swalah. Kwa msemo mwingine yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara alikuwa akitoa Tasliym mbili na mara nyingine akitoa Tasliym moja. Lakini la kwanza ndio lililofanyika mara nyingi. Licha ya kwamba uwezekano huu una umbali kidogo. Kwa sababu Tasliym moja, ijapokuwa imethibiti kutoka kwake, lakini hakuipokea Ibn Mas´uud. Kwa hiyo haidhihiri kuwa ni yenye kuingia katika maneno yake yaliyotajwa:

“Mfano wa Tasliym katika swalah.”

Hadiyth inayo nyingine inayoitolea ushahidi ameipokea Shariyk bin Ibraahiym al-Hajariy ambaye amesema:

“Alituswalisha kama imamu ´Abdullaah bin Abiy Awfaa katika jeneza la msichana wake. Akatulizana kitambo kidogo mpaka tukafikiri kuwa ataleta Takbiyr ya tano. Halafu akatoa Tasliym upande wa kuliani mwake na upande wa kushotoni mwake. Alipomaliza tukamwambia: “Nini mambo haya?” Akasema: “Mimi siwazidishieni juu ya yale niliyomuona nayo Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiyafanya – au alisema – hivi ndivo alivofanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ameipokea al-Bayhaqiy (04/43) na cheni ya wapokezi wake ni dhaifu Ajal al-Hajariy, kama ilivyokwishatangulia katika masuala yaliyotangulia. Pia imesihi kutoka kwake kwa njia nyingine, ambazo baadhi yake zimerufaishwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na zengine zimenasibishwa kwa Swahabah, kama yalivyotangulia huko nyuma. Amepokea Ahmad – kama ilivyo katika “al-Masaa-il” (153) ya Abu Daawuud kutoka kwake – kutoka kwa ´Atwaa´ bin as-Saa-ib ambaye amesema:

“Nilimuona Ibn Abiy Awfaa akiliswalia jeneza ambapo akatoa Tasliym [moja].”

Lakini cheni ya wapokezi wake ni dhaifu. Ndani yake yumo Abu Wakiy´ al-Jarraah bin Maliyh ambaye ni mnyonge na baadhi ya wengine wakamtuhumu.

Hanafiyyah wameonelea suala la Tasliym mbili, kama ilivyokuja katika “al-Mabsuutw” (02/65), Ahmad katika moja ya upokezi kutoka kwake, kama ilivyokuja katika “al-Inswaaf” (02/525), Shaafi´iyyah katika “Sharh Ibn Qaasim-il-Ghazziy” (01/431- Baajuuriy) na akasema: “Lakini imependekezwa kuzidisha:

ورحمه الله وبركاته

“Rehema na baraka za Allaah.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 162-163
  • Imechapishwa: 07/02/2022