82- Kuomba du´aa kati ya Takbiyr ya mwisho na Tasliym ni jambo limewekwa katika Shari´ah. Hilo ni kutokana na Abu Ya´fuur bin ´Abdillaah bin Abiy Awfaa (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Nimemshuhudia akitoa Takbiyr juu ya jeneza nne kisha akasimama kitambo kidogo – yaani akiomba du´aa – kisha akasema: “Mmeniona nikitoa Takbiyr ya tano?” Wakasema: “Hapana.” Akasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoa Takbiyr nne.”

Ameipokea al-Bayhaqiy (04/35) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Kisha akaitoa yeye (04/42, 43), Ibn Maajah (01/457), al-Haakim (01/360), Ahmad (04/383) kupitia kwa Ibraahiym al-Hajariy, kutoka kwa Ibn Abiy Awfaa kwayo, isipokuwa yeye ameirufaisha kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) (na akazidisha baada ya maneno yake: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoa Takbiyr nne kisha husimama kitambo kidogo na akisema yale aliyotaka Allaah ayaseme kisha ndio hutoa salamu.”

al-Haakim amesema:

“Hadiyth hii ni Swahiyh. Ibraahiym hajatiwa kasoro kwa hoja.”

Bali ndivyo. Kwa ajili hiyo adh-Dhahabiy amemkosoa kwa maneno yake:

“Nimesema: “Ibraahiym amedhoofishwa.”

Hilo ni kutokana na ubaya wa hifadhi yake. al-Haafidhw ameashiria hilo katika “at-Taqriyb” kwa kusema:

“Ni mwenye Hadiyth nyonge. Anarufaisha Hadiyth zenye kunasibishwa kwa Swahabah.”

Faida!

01- al-Haafidhw amesema katika “at-Talkhiysw” (1825):

“Baadhi ya wanachuoni wamesema: “Kutofautiana kwa Hadiyth katika du´aa ya kuliombea jeneza inafasiriwa kwamba alikuwa akimuombea maiti kwa du´aa fulani na maiit mwingine du´aa nyingine. Kilichoamrishwa na ule msingi wa du´aa.”

02- ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl al-Awtwaar” (04/55):

“Ikiwa yule anayeswaliwa ni mtoto basi imependekeza mswaliji aombe:

اللهم اجعله لنا سلفا وفرطا وأجرا

“Ee Allaah! Mjaalie awe ni mtangulizi wetu na kuwa na ujira.”

Ameyapokea hayo al-Bayhaqiy kutoka katika Hadiyth ya Abu Hurayrah. Sufyaan amepokea mfano wake katika “Jaamiy´” yake kutoka kwa al-Hasan.”

Hadiyth ya Abu Hurayrah kwa al-Bayhaqiy cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Hapana ubaya kuifanyia kazi katika mfano wa mambo kama haya. Haijalishi kitu hata kama ni yenye kunasibishwa kwa Swahabah muda wa kuwa hajachukulia kuwa ndio Sunnah kiasi cha kwamba dhana ikapelekea kuwa ni yenye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kile ninachochagua mimi ni kwamba mtoto aombewe ile sampuli ya pili kwa sababu ndani yake imekuja:

وصغيرنا… اللهم لا تحرمنا أجره، ولا تضلنا بعده

“… wadogo… Ee Allaah! Usitunyime ujira Wake na wala usitupoteze baada ya yeye kuondoka.”

Imaam Ahmad ameonelea kwamba imesuniwa kuomba du´aa mahala kama hapa. Hayo yamepokelewa na Abu Daawuud” katika “al-Masaa-il” yake (153) kutoka kwake. Hayo pia ndio madhehebu ya ash-Shaafi´iyyah. an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (05/239) amewajengea hoja kutokana na Hadiyth ya al-Hajariy ambayo imeshatajwa hapo juu. Kujengea dalili kwa yaliyoko kabla yake ni yenye nguvu zaidi, pia ni hoja dhidi ya Hanafiyyah pale waliposema:

“Kisha apige Takbiyr ya nne na atoe salamu bila ya kusoma Dhikr yoyote baina yake.”

03- Shaafi´iyyah wameonelea ulazima wa kumuombea maiti du´aa kwa njia isiyofungamana. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyotangulia:

“… amtakasie du´aa.”

jambo ambalo ni haki. Lakini wamemfanya maalum kwa Takbiyr ya tatu na an-Nawawiy amekubali kwamba muhimu ni du´aa yoyote tu pale aliposema (05/236):

“Sehemu ya du´aa hii ni Takbiyr ya tatu na ni jambo lazima ndani yake. Haisihi kwenginepo bila ya tofauti. Kuifanya maalum mahapa hapo ni jambo ambalo hana dalili nalo. Pia wameafikiana kwamba hakuanishwi mahala hapo du´aa.”

Muislamu hatakiwi kusita kuzipa kipaumbele zile du´aa zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zilizokwishatangulia mbele ya zile ambazo zimefanywa kuwa nzuri na baadhi ya watu. Kwani hakika uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo ash-Shawkaaniy amesema (04/55):

“Tambua kwamba katika vitabu vya Fiqh kumejitokeza du´aa mbali na zile zilizopokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lililo na haki zaidi ni kushikamana na kilichothibiti kutoka kwake.”

Bali mimi naamini kuwa jambo hilo ni lazima kwa yule mwenye utambuzi wa kile kilichopokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani katika hali hiyo kukiendea kingine badala yake kunachelea juu ya mtu huyo kuingia ndani ya maneno Yake (Tabaarak wa Ta´ala):

قَالَ أَتَسْتَبْدِلُونَ الَّذِي هُوَ أَدْنَىٰ بِالَّذِي هُوَ خَيْرٌ

“Je, hivi mnataka kubadilisha yaliyo duni kwa yaliyo bora?”[1]

[1] 02:61

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 159-161
  • Imechapishwa: 07/02/2022