82. Hakuna yeyote amuonae Allaah duniani


Duniani hakuna yeyote awezaye kumuona. Mtu hawezi kumuona Allaah kutokana na utukufu Wake. Hakuna yayote duniani awezaye kumuona Allaah. Hata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipopandishwa safari ya mbinguni hakumuona licha ya kuwa alimkaribia. Aliulizwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama alimuona Mola wake, akajibu:

“Ni nuru. Nitamuonaje?”

Bi maana pazia Yake ni nuru na ndio maana sikuweza kumuona. Hakuna yeyote hapa duniani awezaye kumuona. Ama Aakhirah atawatunuku waumini na kuwapa nguvu za kuweza kumuona. Lau atajidhihirisha mbele ya yeyote duniani basi atakufa. Wakati Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kusikia maneno ya Mola wake, akataka pia kumuona na akasema:

رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْك

“Mola wangu! Nionyeshe ili nikutazame.”[1]

Kwa sababu alitamani kumuona Mola wake. Allaah akajibu:

لَن تَرَانِي

“Hutoniona.”[2]

Bi maana duniani.

لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي

“(Lan) Hutoniona! Lakini tazama jabali. Likitulia mahali pake, basi utaniona.”[3]

Mlima ukasambaratika na ukawa changarawe kutokana na utukufu wa Allaah.

وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا

“… na Muusa akaanguka hali ya kuzimia.”[4]

Pamoja na kwamba hakumuona Mola wake akazimia kutokana na ukubwa wa khofu. Allaah alitaka kumbainishia kwamba hakuna yeyote amuonae wala awezaye kumuona hapa duniani.

[1] 7:143

[2] 7:143

[3] 7:143

[4] 7:143

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 61-62
  • Imechapishwa: 18/08/2021