81. Baada ya kufufuliwa watu watahesabiwa na kulipwa

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Baada ya kufufuliwa watahesabiwa na watalipwa kwa matendo yao. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

“Na ni vya Allaah pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili awalipe wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda na awalipe wale waliofanya wema kwa yaliyo mazuri zaidi.” (an-Najm 53 : 31)

MAELEZO

Baada ya kufufuliwa watu watalipwa na watahesabiwa kwa matendo yao. Waliofanya kheri, watalipwa kheri, na waliofanya uovu, watalipwa uovu. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

”Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe ya atomu ataiona, na yule atakayetenda uovu uzito wa chembe ya atomu ataiona.” (az-Zalzalah 99 : 07-08)

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Tutaweka mizani za uadilifu siku ya Qiyaamah, hivyo basi haitodhulumiwa nafsi yoyote ile kitu chochote. Na japokuwa ni uzito wa mbegu ya hardali, tutaileta. Na inatosheleza Kwetu kuwa Wenye kuhesabu.” (al-Anbiyaa´ 21 : 47)

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ

“Atakayekuja kwa  jema, basi atalipwa [thawabu] kumi mfano wa hilo, na atakayekuja kwa uovu, basi hatolipwa isipokuwa mfano wa hilo, nao hawatodhulumiwa.” (al-An´aam 06 : 160)

Jema moja hulipwa mara kumi kwenda mpaka mara mia saba na zaidi ya hapo – ni fadhilah na neema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwanza Yeye (Jalla wa ´Alaa) amejifadhilisha juu ya mja kwa kitendo chema, kisha baada ya hapo amejifadhilisha mara nyingine kwa thawabu hii iliopana na kubwa. Ama kuhusu kitendo kiovu, kinalipwa kwa mfano wake pasi na adhabu kuwa kubwa. Amesema (Ta´ala):

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ

“Atakayekuja kwa  jema, basi atalipwa [thawabu] kumi mfano wa hilo, na atakayekuja kwa uovu, basi hatolipwa isipokuwa mfano wa hilo, nao hawatodhulumiwa.” (al-An´aam 06 : 160)

Hili ni katika ukamilifu wa fadhilah na wema wa Allaah.

Shaykh ametumia dalili ya hilo kwa maneno Yake (Ta´ala):

لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُو

“… ili awalipe wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda… “

Hakusema kuwalipa maovu zaidi kama alivosema juu ya wale wengine:

وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

“… na awalipe wale waliofanya wema kwa yaliyo mazuri zaidi.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 144-145
  • Imechapishwa: 04/06/2020