81. Aina mbili ya uombezi


Uombezi kwa Allaah kwa kutimia sharti hizi mbili ni haki. Huu ndio uombezi wenye kuthibitishwa. Kuhusu uombezi wenye kukanushwa ni uombezi juu ya makafiri. Kwa msemo mwingine ni ule uombezi unaokuwa pasi na idhini ya Allaah. Wanachuoni wamesema kuwa kuna uombezi aina mbili:

Ya kwanza: Uombezi wenye kuthibitishwa.

Ya pili: Uombezi wenye kukanushwa. Amesema (Ta´ala):

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wowote wa waombezi.” (74:48)

مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ

“Madhalimu hawatokuwa na rafiki wa dhati na wala mwombezi anayetiiwa.” (40:18)

Anaweza akaja mtu na kukwambia kuwa uombezi haukubaliwi kutokana na dalili hizi mbili. Mjibu kwa kumwambia kuwa kuna Aayah zinazotolea dalili kuthibitisha uombezi. Amesema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake.” (02:255)

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“Na wala hawamuombei uombezi yeyote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.” (21:28)

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

“Malaika wangapi mbinguni hautowafaa chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa amtakaye na akaridhia.” (53:26)

Hizi ni dalili zinazofahamisha kuwa uombezi unakubaliwa kwa kutimia sharti mbili; idhini ya Allaah na amridhie yule mwenye kuombewa. Sio uombezi wote ni wenye kuthibitishwa kama ambavyo vilevile sio uombezi wote ni wenye kukanushwa. Mambo yanatakiwa kupambanuliwa kwa mujibu wa vile zilivyofahamisha dalili.

Qur-aan haigonganishwi sehemu kwa nyingine. Kinachotakiwa ni kuoanisha baina ya Aayah, kufasiri baadhi kwa zengine, kuzipa nguvu baadhi kwa zengine. Huu ndio mfumo wa wale waliobobea katika elimu. Hakuchukuliwi upande mmoja na kusema kuwa uombezi umethibiti kwa watu wote. Hivi ndivyo wanavosema waabudu makaburi na washirikina wa hapo kale. Amesema (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah visivyowadhuru na wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”” (10:18)

Wanaomba uombezi ilihali wanamshirikisha Allaah. Huu ndio uombezi batili wenye kukataliwa.