8. Tofauti kati ya Zuhd (kuipa nyongo dunia) na madhehebu ya Suufiyyah

Ndugu wapendwa! Uislamu unaamrisha kuwa na msimamo wa kati na kati katika mambo yote ili kusiwepo yeyote atakayepetuka mipaka wala kuzembea yaliyoamrishwa. Kadhalika Uislamu kwa nisba ya kuipa nyongo dunia (az-Zuhd) uko kati na kati baina ya tamaa za mayahudi, upupiaji na mapenzi ya kupindukia kuipenda dunia na baina ya watawa wa wakristo ambao wamejiepusha kabisa na kufanya sababu za kupata riziki kama jinsi wanavyojiepusha vilevile na kufanya kazi na kutafuta chumo

Jambo la kuipa nyongo dunia ikiwa litafanywa ndani ya mipaka iliyowekwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi huchukuliwa ni kitu chenye kusifiwa katika Uislamu. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuipa nyongo dunia na kujiepusha na starehe za dunia, kadhalika Abu Bakr, ´Umar na Maswahabah wengine wengi. Lakini hata hivyo kuipa kwao nyongo dunia haikuwa na maana ya kujiepusha na kukaa chini wakisubiri watu wengine ndio waje na kuwapa. Bali watu walikuwa wakiwajia na mazawadi ambayo wanayapokea na kuyatoa katika njia za kheri. Hawakuwa wakiacha vitu vizuri isipokuwa pale ambapo ambapo itakuwa ni vigumu kuvipata. Pindi wanapovipata basi wanaburudika navyo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akipenda wanawake na manukato na kadhalika nyama, mara akifunga, mara akila, akilala, akifanya kazi, akipambana Jihaad, akihukumu kati ya waislamu, akiwafunza Qur-aan na mambo mengine ya kheri.

Kulipatikana vilevile baadhi katika wanachuoni ambao waliipa nyongo na kutojishughulisha na mambo ya dunia hii kama jinsi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyokuwa akifanya. Hata hivyo aina hii ya kuipa nyongo dunia ambayo ilikuwa ikifanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sio wajibu kwa Waislamu, kwa sababu haikuamrishwa katika Qur-aan wala Sunnah. Dalili nyingine ni kwamba kulikuwepo Maswahabah ambao walikuwa wanajishughulisha na biashara na kukusanya utajiri mkubwa. Miongoni mwao ni ´Uthmaan bin ´Affaan, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf na az-Zubayr bin al-´Awaam. Answaar walikuwa na mabustani mawili makubwa ambapo wakifanya kazi ndani yake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwakataza kufanya hivo. Bali imepokelewa katika Hadiyth kwamba amesema:

“Neema ya mali nzuri ni ya yule mtu ambaye ni mwema.”[1]

Alimuombea du´aa mtumishi wake Anas bin Maalik na kumalizia Du´aa yake kwa kusema:

“Ee Allaah! Mkithirishie mali yake na wana wake na mbariki navyo.”[2]

Ama kuhusiana na Zuhd ya Suufiyyuun, ina maana ya mtu kuacha kuchuma mapato ya halali, kufanya kazi zenye manufaa na mtu kukaa chini katika hali ya kusubiri vile atavyoletewa na watu, kuombaomba, kuwataka msaada watu na kuwatembelea mara nyingi watawala na wafanya biashara ili kuwahadaa pamoja na kuwasifu na kuwatapa ili aweze kupata makombo ya chakula yanayobaki juu ya meza. Vivyo hivyo inahusiana na kujidhihirisha ufakiri wa kiongo kwa mavazi yake. Wanavaa mavazi ya zamani na mavazi ya kuchanika ili kujionyesha kuwa wanaipa nyongo dunia na kwamba ni wachaji Allaah na kwamba ni mawalii wa Allaah. Baadhi yao wanaweza kuwa wakweli juu ya uvumilivu wa matatizo ya kujitakia mwenyewe na matokeo yake wakakaa masiku mengi pasi na kula au akala mkate mkavu tu na chumvi ilihali ni mwenye uwezo wa kula vyakula vizuri. Kwa hali yoyote ile, hili linakwenda kinyume na Sunnah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Anayezipa mgongo Sunnah zangu si katika mimi.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kula nyama na kadhalika kondoo aliyenona, wakati baadhi ya Suufiyyuun wanapetuka mipaka kwa kiasi ambacho wanakula vitu vyenye kuwadhuru. Baadhi yao wanaweza kula majivu, udongo na wanapendelea kunywa maji machafu badala ya maji masafi na ya baridi, kwa hoja ya kwamba hawawezi kuyatekelezea shukurani zake. Hoja hii ni ya kipuuzi. Wakiacha maji ya baridi, ina maana ya kwamba watakuwa wamemtekelezea Allaah shukurani kwa neema zingine ambazo Allaah Amewatunuku; kama mfano wa kuona, kusikia, afya njema na nyenginezo? Bali anayefanya jambo kama hilo anatenda madhambi kwa kuwa anajitia mwenyewe katika jambo ambalo lina madhara katika mwili wake na linapelekea katika kumuua. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا

“Wala msiziue nafsi zenu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwahurumia.” (an-Nisaa´ 04:29)

Vilevile Amesema (Ta´ala):

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

“Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu.” (al-Baqarah 02:185)

Vilevile imeruhusiwa kwa msafiri au Muislamu mgonjwa kutofunga Ramadhaan, jambo ambalo ni Rahmah kwetu – himdi zote njema ni Zake Allaah kwa neema Zake.

Uvumilivu juu ya matatizo ya mtu kujitakia mwenyewe yalikuwepo kati ya Suufiyyuun wa mwanzoni, ama Suufiyyuun waliokuja nyuma hamu yao kubwa ikawa ni kula na kunywa. Baada ya kukosoa matatizo ya Suufiyyuun ya kujitakia wenyewe na kuipa nyongo dunia kwa kiasi cha kupindukia, na likapelekea katika kujitesa nasfi zao, Ibn-ul-Jawziy akasema katika “Talbiys Ibliys”:

“Kuipa nyongo dunia kwa sampuli hii ambayo inavuka mipaka na ambayo tumekatazwa kuifanya, Suufiyyuun wa zama zetu wameigeuza. Wamekuwa ni waroho wa vyakula kama jinsi wenzao waliowatangulia walivyokuwa katika njaa. Wanapiga chakula cha mchana, chakula cha joni, vitu tamtam na vyote hivyo, au kwa uchache vingi katika hivyo, wanavichuma kwa pesa za haramu. Wameacha kutafuta machumo ya halali na wakaipa ´ibaadah mgongo na wakakaa bila kufanya kazi. Matokeo yake wengi wao wakawa hawana hamu nyingine zaidi ya kula, kunywa na kucheza.”

Yale yaliyosimuliwa na Ibn-ul-Jawziy ndio hali pia ya Suufiyyuun hivi leo, bali wamewazidi kwa maradufu. Ndugu! Hakuna muda wa kutosha ili kuweza kutaja matendo ya Suufiyyuun kuhusiana na suala hili.

[1] Swahiyh. Ameipokea Ahmad.

[2] al-Bukhaariy (6344).

[3] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqiyqat-us-Suufiyyah
  • Imechapishwa: 24/12/2019