Allaah (Ta´ala) mwenyewe ameeleza ni watu gani wanaostahiki kupewa zakaah pale aliposema:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Hakika swadaqah ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao [katika Uislamu] na kuwakomboa watumwa na wenye deni na katika njia ya Allaah na msafiri [aliyeharibikiwa]. Ni faradhi itokayo kwa Allaah. Na Allaah ni Mjuzi, Mwenye hikmah.” (09:60)

Ni watu nane.

Mosi: Mafukara ni wale wasiopata cha kuwatosheleza mnamo nusu ya mwaka. Ikiwa mtu hana cha kumtosheleza kujilisha mwenyewe na familia yake mnamo miezi sita basi anazingatiwa kuwa ni fakiri. Apewe kinachomtosheleza yeye na familia yake kwa mwaka mmoja.

Pili: Masikini ni wale wenye kupata cha kuwatosheleza chini chini kwa nusu ya mwaka lakini si kwa mwaka mmoja. Wapewe cha kuwatosheleza kwa mwaka. Ikiwa mtu hana pesa lakini ana pato analolipata kwa njia nyingine kama kazi, mshahara au utumiaji fursa na kinamtosheleza, basi hana haki ya zakaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haijuzu kumpa swadaqah tajiri wala aliye na nguvu ambaye anaweza kuchuma riziki yake.”[1]

Tatu: Wale wenye kuikusanya. Watu hawa wameteuliwa na mtawala mkuu wa nchi. Kazi yao wao ni kukusanya zakaah, kuwapa wale wanaoistahiki, kuihifadhi na mengineyo. Wanatakiwa kupewa sehemu katika zakaah kutokana na kazi yao hata kama watakuwa ni matajiri.

Nne: Wale watu ambao nyoyo zao zinataka kulainishwa. Hawa ni wale machifu wa makabila ambao mioyo yao haina imani yenye nguvu. Wapewe zakaah ili mioyo yao iwe na nguvu ili waweze kulingania katika Uislamu na wawe viigizo vyema.

Je, mtu asiyekuwa msomi mwenye imani dhaifu ana haki ya kupewa zakaah ili aweze kuwa na nguvu? Baadhi ya wanachuoni wanaonelea hivyo kwa sababu maslahi ya kidini ni yenye nguvu zaidi kuliko maslahi ya kimwili. Ikiwa fakiri anapewa kitu ili kufanya mwili wake uwe na nguvu, basi ni jambo lenye kufaa zaidi kupewa kitu chenye kufanya imani yake kuwa na nguvu. Wanachuoni wengine hawaonelei hivyo kwa sababu kufanya imani ikawa na nguvu ni jambo la kibinafsi.

Tano: Watumwa. Mtumwa anunuliwe na aachwe huru, mtumwa anayejaribu kujiacha huru achangiwe pesa na watumwa wa Kiislamu waachwe huru.

Sita: Wenye deni. Ikiwa hawezi kulipa deni lake apewe zakaah ili aweze kulilipa. Haijalishi kitu sawa deni likiwa kubwa au dogo. Hata kama yule mwenye kudaiwa na familia yake ni tajiri na wana riziki ya kuwatosheleza, wana haki ya kupewa katika zakaah ili aweze kulipa deni lake. Hata hivyo haijuzu kuangusha [kuachia lile] deni la mdaiwa fakiri kwa kunuia kuwa hiyo ndio zakaah yake.

Je, inajuzu kumpa zakaah mdaiwa ili aweze kulipa deni lake ikiwa ni baba au mtoto? Wanachuoni wametofautiana juu ya hilo. Maoni sahihi ni kuwa inajuzu.

Inajuzu pia kwa mtoa zakaah kulipa deni pasina yule mwenye kudaiwa kujua hilo kwa sharti mlipaji awe ni mwenye kujua kuwa mdaiwa hana uwezo wa kulilipa.

Saba: Katika njia ya Allaah ni Jihaad katika njia ya Allaah. Wapambanaji wapewe zakaah watayotumia wakati wa Jihaad ili kununua silaha na vinginevyo.

Miongoni mwa njia ya Allaah ni pamoja vilevile na elimu ya Kishari´ah. Mwanafunzi ana haki ya kupewa zakaah ili aweze kununua vile vinavyohitajika katika masomo katika madaftari na vinginevyo. Isipokuwa tu ikiwa kama ni tajiri na anaweza kupata hayo kwa hali yoyote.

Nane: Mtangaji. Ni msafiri aliyekwama njiani. Ana haki ya kupewa zakaah ili aweze kufika nyumbani.

Hawa ndio wanaostahiki kupewa zakaah ambao Allaah (Ta´ala) amewataja katika Kitabu Chake. Ni faradhi yenye kutokamana na ujuzi na hekima – na Allaha ni Mjuzi wa yote, Mwingi wa hekima.

Haijuzu kutoa zakaah katika mambo mengine kama kujenga misikiti na kutengeneza barabara. Kwa sababu Allaah ametaja wale wenye kuistahiki kwa njia ya ukomo ikiwa na maana kuwa haijuzu kuitoa kwa wengine.

Tukitafakari watu hawa wenye kuiistahiki, basi tutaona kuwa kuna ambao wanahitajia zakaah wao wenyewe na wengine waislamu wanaihitajia. Kwa hivyo tunapata kujua hekima ya uwajibu wa zakaah. Zakaah inajenga jamii njema, iliokamilika na nzuri kadiri na uwezekano. Uislamu haupuuzii mali na maslahi yaliyojengwa juu ya mali. Uislamu haukumwacha bakhili na mchoyo atumie mali yake huru kutokana na matamanio yake. Hakuna kitu kinachoelekeza katika mema na kuzitengeneza hali za watu kama Uislamu – na himdi zote ni za Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] Ahmad (3/56), Abu Daawuud (1636), an-Nasaa’iy (2598), Ibn Maajah (1841) na al-Haakim (1/407) aliyesema kuwa Hadiyth iko kwa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 19-21
  • Imechapishwa: 05/06/2017