Huenda mtu akasema kuna Bid´ah ambazo waislamu wamezipokea na kuzitendea kazi. Bid´ah hizo hazikuwepo kipindi cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baadhi ya Bid´ah hizo ni masomo na uchapishaji wa vitabu. Bid´ah hizi waislamu wamezisifu na kuzifanyia kazi na kuonelea kuwa ni katika matendo mazuri kabisa. Ni vipi basi tutaoanisha matendo haya ambayo kunakaribia kutokuwepo maoni tofauti juu yake na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ninakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kitakachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”?

Jawabu langu ni kuwa matendo haya sio Bid´ah; ni njia zenye kupelekea katika mambo yaliyowekwa katika Sharia´h. Njia zinatofautiana kwa kutegemea zama na maeneo. Kitendo kikiwa kimewekwa katika Shari´ah basi njia yake pia itakuwa inafaa na kitendo kikiwa hakikuwekwa katika Shari´ah basi njia yake pia itakuwa haifai. Chenye kupelekea katika haramu pia ni haramu. Bali kitendo cha kheri chenye kupelekea katika shari itakuwa ni shari na ni chenye kukatazwa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَا تَسُبُّوا الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ فَيَسُبُّوا اللَّـهَ عَدْوًا بِغَيْرِ عِلْمٍ

“Na wala msiwatukane wale wanaowaomba asiyekuwa Allaah; wasije nao kumtukana Allaah kwa uadui bila ya kujua.”[1]

Kuwatukana waungu wa washirikina si jambo la kimakosa; bali ni haki na jambo linalotakikana. Lakini jambo la kutukanwa Allaah ni makosa makubwa sana. Pamoja na kuwa ni jambo lenye kusifiwa kuwatukana miungu ya washirikina inapelekea Allaah kutukanywa, ikawa ni haramu na imekatazwa kuwatukana. Nayataja haya ili kutoa dalili kuonyesha kuwa njia zina hukumu moja kama malengo. Hata kama masomo na uchapishaji wa vitabu uliyopo hii leo ni uzushi ambao haukuwepo wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini hata hivyo sio malengo; bali ni njia – na njia zina hukumu moja kama malengo. Kutokana na hili endapo mtu atajenga masomo ili kufunza ndani yake somo la haramu ujenzi utakuwa ni haramu wakati kujenga masomo ili kufunza ndani yake masomo yaliyowekwa katika Shari´ah ujenzi utakuwa unafaa.

[1] 06:108

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ibdaa´ fiy Kamaal-ish-Shar´ wa Khatwar-il-Ibtidaa´, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 23/10/2016