Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Katika Sunnah hakuna kipimo [Qiyaas].”

Bi maana katika dini ya Allaah hakuna kipimo. Wakati Allaah anaposema kitu basi mwanaadamu hana lolote la kusema. Kunapowekwa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah vipimo vinakoma. Dalili haitakiwi kukabiliwa na akili, kipimo, maoni wala kitu kingine. Hatuna jengine isipokuwa kujisalimisha:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe kuwa mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao kisha wasipate katika nyoyo zao kipingamizi katika yale uliyohukumu na wajisalimishe ukweli wa kujisalimisha.”[1]

Baadhi ya watu wanatumia vipimo kwa kiasi cha kwamba wanafikia mpaka kurudisha dalili ya Qur-aan na Sunnah. Wanasema kuwa dalili hii inaenda kinyume na misingi na kipimo. Kwa msemo mwingine watu hawa wanapindukia. Imaam Ahmad anaashiria watu hawa. Vinginevyo kunaweza kuwepo kipimo cha sawa. Lakini hata hivyo kipimo ni kama nyamafu; mtu anaila tu wakati wa dharurah. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika kijitabu chake kinachoitwa “Ma´aarij-ul-Wusuul”:

“Kupitia usomi imeonekana kuwa hakuna maafikiano yoyote juu ya jambo fulani isipokuwa kuna dalili yake katika Qur-aan na Sunnah.”

Vivyo hivyo kipimo; hakuna kipimo chochote isipokuwa tayari kimekwishatolewa dalili katika Qur-aan na Sunnah. Pamoja na hivyo watu wanatofautiana inapokuja katika kuzizunguka dalili zote. Ni watu wachache wanaozizunguka dalili zote au karibu zote. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) alikuwa ni mmoja katika wachache hao. Ndio maana utaona jinsi wanazuoni wengi wanavotumia vipimo vya sawa. Ni kitu ambacho Allaah amewaongoza kwacho. Lakini hata hivyo lau mtu angelibobea zaidi katika Sunnah basi angelipata dalili. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha mambo ya msingi na ya matawi na hakuacha kitu bila ya kukisema:

مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ

“Hatukusuru katika Kitabu kitu chochote.”[2]

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na Nimekutimizieni neema Yangu na Nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.”[3]

Dini yetu imekamilika. Hakuna upungufu ndani yake. Baadhi ya watu wanafanya Ijtihaad na kutumia vipimo sahihi vinavyoafikiana na dalili. Lakini hata hivyo katika masuala hayo kuna dalili ambazo hazikuwafikia. Lau wangelifikiwa na dalili wangelizitumia kama hoja na kuachana na kipimo. Mtu mwenye kudurusu Sunnah kwa kina – kama Ibn Taymiyyah – anakuja kugundua kuwa maafikiano haya yalikuwa na dalili katika Qur-aan na Sunnah. Maafikiano yao ni sahihi na yanaafikiana na dalili katika Qur-aan na Sunnah. Lau wangelifikiwa na dalili wangeliitumia kama hoja. Lakini hawakufanya hivo. Wanachuoni kama Ibn Taymiyyah kupitia usomi wameona kuwa kuna maafikiano na vipimo sahihi ambavyo tayari vimekwishathibitishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini kama tulivyosema kuna Hadiyth kutoka kwa Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo hazikuwafikia wanachuoni.

Kwa hali yoyote Imaam Ahmad alikuwa mkali kabisa inapokuja katika vipimo. Mara nyingi alikuwa akikemea mambo yanayodaiwa kuwa na maafikiano na kusema:

“Unajuaje kama hakuna mwengine mwenye kuonelea kinyume?”

Alikuwa anapenda badala yake mtu aseme:

“Sijui kama kuna mwengine mwenye kuonelea kinyume juu ya suala fulani.”

Mtu asisemi kuwa Ummah umeafikiana juu ya kitu fulani. Lililo salama ni mtu kusema kuwa hajui tofauti yoyote. Kwa sababu siku zote kunaweza kuwa tofauti ambayo haijui.

[1] 04:65

[2] 06:38

[3] 05:03

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 370-371
  • Imechapishwa: 23/07/2017