79. Allaah ameikamilisha dini kupitia Muhammad (صلى الله عليه وسلم)

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah kupitia kwake ameikamilisha dini. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (al-Maaidah 05 : 03)

MAELEZO

Dini yake (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) ni yenye kubaki mpaka siku ya Qiyaamah. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufariki isipokuwa baada ya kubainishia Ummah wake yale yote wanayohitajia. Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuacha hata yule ndege ambaye huruka kwa mbawa zake angani, isipokuwa ametutajia kitu katika elimu yake.”[1]

Kuna mshirikina mmoja alisema kumwambia Salmaan al-Faarisiy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mtume wenu amewafundisha mpaka namna ya kukidhi haja.” Akasema: “Ndio. Ametukataza kuelekea Qiblah wakati tunapofanya haja kubwa au ndogo. Ametukataza vilevile kujisafisha chini ya mawe matatu, mkono wa kulia, kinyesi au mfupa.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha dini yote. Amefanya hivo ima kwa maneno yake, kitendo chake, kulikubali kwake jambo au kwa kujibu kwa swali. Jambo kubwa na muhimu zaidi alichobainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni Tawhiyd.

Kila alichokiamrisha ni kheri kwa Ummah juu ya Aakhirah na maisha yao. Kila alichokikataza ni shari kwa Ummah juu ya Aakhirah na maisha yao. Baadhi ya watu wajinga wanadai kuwa kuna ufinyu na ugumu katika dini. Hilo linatokana na akili yao pungufu, uchache wa subira na udhaifu wa imani. Vinginevyo kanuni yenye kuenea inasema kuwa Allaah hakutufanyia uzito wowote katika dini na kwamba dini yote ni nyepesi na sahali. Allaah (Ta´ala) amesema:

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

“Allaah anakutakieni mepesi na wala hakutakieni magumu.” (al-Baqarah 02 : 185)

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ

“Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika dini.” (al-Hajj 22 : 78)

مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ

”Allaah hataki kukufanyieni magumu wowote.” (al-Maaidah 05 : 06)

Himdi zote njem ni stahiki ya Allaah juu ya kututimizia neema Zake na kuikamilisha dini Yake.

[1] Ahmad (5/163).

[2] Muslim (262).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 142-143
  • Imechapishwa: 03/06/2020