78. Uwajibu wa kuhukumu kwa Shari´ah katika nyanja zote

Vilevile kuhukumiana kwa Allaah katika kuamrisha mema na kukataza maovu. Kwa sababu Allaah kaamrisha kutiiwa na amekataza kuasiwa. Kitendo cha watu kuachwa na hawakemewi, hawaamrishwi na wala hawakatazwi, huku ni kuiharibu hukumu ya Allaah (Ta´ala). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule katika nyinyi atakayeona maovu, basi ayakemee kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa ulimi wake. Asipoweza, basi afanye hivo kwa moyo wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”[1]

Kuhukumu kwa Allaah kunakuwa mpaka katika mambo ya tofauti ambayo ni chini ya shirki na kufuru. Ni lazima kubainisha hukumu ya Allaah ndani yake na kubainishwe ni ipi utiifu, maasi, mema, maovu na lilazimishwe hilo. Vilevile achukuliwe hatua yule mwenye kwenda kinyume mpaka jamii isalimike kutokamana na maangamivu. Ama kukiachwa suala la kuamrisha mema na kukataza maovu, hakika hii ni sababu ya kuiangamiza jamii yote; mwema na muovu. Watu wakiona maovu na hayakatazwi, basi kunakhofiwa Allaah akateremsha adhabu kutoka Kwake.

[1] Ameipokea Muslim (78), at-Tirmidhiy (2172), an-Nasaa´iy (5008) na (Ibn Maajah (1275).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 106-107
  • Imechapishwa: 19/11/2018