78. Neno moja la mzaha linaweza kumfanya mtu akaritadi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Yaweza kusemwa pia: “Wale ambao Allaah Kasema kuwahusu:

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ

“Wanaapa kwa jina la Allaah kwamba hawakusema [neno la kufuru] na hali wamekwishasema neno la kufuru na wakakufuru baada ya Uislamu wao.” (09:74)

Hamkusikia ya kwamba Allaah kawakufurisha kwa sababu ya neno moja tu, pamoja na kuwa walikuwa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakipigana jihaad pamoja naye, wakiswali pamoja naye, wakitoa zakaah pamoja naye, kuhiji na wakimpwekesha Allaah? Hali kadhalika wale ambao Allaah amesema kuwahusu:

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Na ukiwauliza, bila shaka watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema: “Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”” (09:65-66)

Watu hawa ambao Allaah ameweka wazi ya kwamba wamekufuru baada ya kuamini kwao – pamoja na kuwa wako na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk – walisema maneno ambayo walisema kuwa waliyasema kwa mzaha tu. Fikiria hoja tata hii pale wanaposema:

“Je, mnawakufurisha Waislamu ambao wanashuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah, wanaswali na wanafunga?”

Kisha fikiria jibu lake. Kwa hakika ni katika yamanufaa yaliyomo kwenye waraka huu.

MAELEZO

Hili ni jibu la saba ambalo lina malengo mawili:

1 – Allaah (Ta´ala) amewahukumu wanafiki kuwa ni makafiri baada ya kutamka tamko la kufuru. Haya pamoja na kwamba walikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanaswali, wanatoa zakaah, wanahiji, wanatoka katika jihaad na wanampwekesha Allaah.

2 – Amewahukumu wanafiki kuwa ni makafiri kwa sababu ya kumchezea shere Allaah, Aayah Zake na Mtume Wake. Walisema:

“Hatujapata kuona watu kama wasomi wetu hawa ambao ni waroho, waongo na ni waoga sana wakati wa mapambano.”[1]

Walikuwa wakimaanisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Ndipo Allaah akateremsha:

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Na ukiwauliza, bila shaka watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.””

Wamehukumiwa kuwa ni makafiri baada ya kuamini kwao, licha ya kuwa walisema kwamba walikuwa wanatania tu na kwamba hawakuwa wakimaanisha kweli. Walikuwa wanaswali na wanatoa zakaah. Baada ya hapo mtunzi (Rahimahu Allaah) akasema kuwa jibu ya utata huu ni miongoni mwa majibu yenye manufaa kabisa yaliyo kwenye waraka huu.

[1] Ibn Jariyr at-Twabariy, mjeledi. 14, na Ibn Kathiyr (02/381).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 88-89
  • Imechapishwa: 25/11/2023