78. Ataingia Peponi mwanzoni au mwishoni

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Yule ambaye Allaah atamwadhibu kwa Moto Wake, basi atamtoa nje kutokana na imani yake. Kisha atamwingiza Pepo Yake:

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe ataiona.”[1]

MAELEZO

Ambaye huko Aakhirah ataadhibiwa kutokana na dhambi yake kubwa basi Allaah atamtoa nje ya Moto na badala yake kumwingiza Peponi. Kutokana na imani yake na kule kumwabudu kwake Allaah pekee ataingia Peponi ima pale mwanzoni tu au mwishoni. Ama kafiri na mshirikina hakuna matumaini kwao ya kuingia  Peponi au kupata huruma ya Allaah. Hakuna watakaodumishwa Motoni milele isipokuwa washirikina na makafiri peke yao. Kuhusu waislamu watenda madhambi, hata kama wataingia Motoni na kuadhibiwa ndani yake, watatolewa pale mwanzoni au mwishoni na wataingia Peponi. Maneno ya mtunzi:

“… kutokana na imani yake.”

analenga kumpwekesha Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe ataiona, na yule atakayetenda shari uzito wa chembe ataiona.”[2]

Mtu atakutana na yale aliyoyafanya, ni mamoja ni mema au maovu:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا

“Hakika Allaah hadhulumu uzito wa atomu. Na ikiwa ni [kitendo] kizuri hukizidisha na hutoa kutoka kwake ujira mkubwa.”[3]

Licha ya hivo matendo maovu hayalipwi maradufu isipokuwa yanalipwa kama yalivyo:

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ

“Atakayekuja kwa jema moja, basi atapata [thawabu] kumi mfano wake, na atakayekuja kwa ovu, basi hatolipwa isipokuwa mfano wake – nao hawatodhulumiwa.”[4]

Ni jambo linaenda kinyume na uadilifu wa Allaah (´Azza wa Jall) akatenda ovu moja na akamwadhibu kwa maovu mengi. Mtenda dhambi akiwa ni muislamu kuna uwezekano vilevile wa Allaah kumsamehe. Kwa sababu kuadhibiwa kwa dhambi ni uadilifu kutoka kwa Allaah, kulipwa maradufu kwa mema ni fadhilah kutoka kwa Allaah. Licha ya kwamba maovu hayaongezwi lakini yanaweza kuwa khatari zaidi kutokana na utukufu wa wakati (kama mfano wa Ramadhaan au miezi ya kuhiji) au maeneo matakatifu (kama mfano wa Haram), lakini hata hivyo hayaongezwi. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu kufanya dhambi Haram:

وَمَن يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍ بِظُلْمٍ نُّذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ

“Na yeyote anayekusudia ndani yake kufanya upotevu kwa dhuluma tutamuonjesha adhabu iumizayo.”[5]

Kutokana na utukufu wa wakati na kukiuka heshima ya maeneo matakatifu, basi dhambi inaweza kufanywa khatari zaidi.

[1] 99:07-08

[2] 99:07-08

[3] 04:40

[4] 6:160

[5] 22:25

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 17/08/2021