78. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya waislamu waliokufa katika dhambi kubwa


Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

30- Sema “Allaah mtukufu atawatoa kwa fadhila Zake

     kutoka Motoni viwiliwili vilivyoungua

31- [Viwekwe] kwenye mto wa Firdaws ambapo vitapata uhai kwa maji yake

     kama kokwa lililobeba mbegu

MAELEZO

Haya ni masuala kuhusu watenda maasi wanaomuabudu Allaah peke yake ambao wana madhambi makubwa chini ya shirki. Hawa wanazingatiwa kuwa ni waumini na wapwekeshaji. Lakini imani na Tawhiyd yao ni pungufu. Licha ya hivyo hawatoki katika Uislamu tofauti na wanavyoonelea Khawaarij na Mu´tazilah. Wako chini ya matakwa; iwapo Allaah atataka atawasamehe na hatowaadhibu na wataingia Peponi kipindi kile cha kwanza, na Allaah vilevile akitaka atawaadhibu. Lakini ikibidi hivo hawatodumishwa Motoni milele kama watavyodumishwa makafiri na washirikina. Watatolewa ndani ya Moto baada ya kuadhibiwa. Hilo litapitika ima kutokana na uombezi wa waombezi, fadhila za Allaah (´Azza wa Jall) au kwa kuisha kwa adhabu yao. Hawatodumishwa Motoni milele kabisa.

Motoni ataingia kafiri na mshirikina. Kuna uwezekano vilevile muumini na muislamu anayemuabudu Allaah peke yake akaingia humo kutokana na madhambi yake. Lakini kafiri na mshirikina watadumishwa Motoni. Kuhusu mpwekeshaji na muumini hawatodumishwa humo milele ikiwa kama wataingia. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah tofauti na wanavyoonelea Khawaarij na Mu´tazilah.