77. Uwajibu wa kuhukumu kwa Shari´ah katika ´ibaadah

Hali kadhalika ni lazima kuhukumu kwa Shari´ah katika mambo ya ´ibaadah mbalimbali. Kwa sababu ziko ´ibaadah zinazotembea kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Hizi ndio ´ibaadah sahihi. Upande mwingine ziko ´ibaadah zimezozushwa na hazina msingi wowote katika Qur-aan na Sunnah. Hizi ni Bid´ah na ni wajibu kubainisha ubatili wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amelibainisha hilo na akapambanua pale aliposema:

“Atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, atarudishiwa.”

“Tahadharini na mambo ya kuzua! Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”

Ni lazima kutumia hukumu ya Allaah katika mambo mbalimbali ya ´ibaadah. Yanayoafikiana na Qur-aan na Sunnah ndio sahihi. Yanayokwenda kinyume na Qur-aan na Sunnah ni batili. Haijuzu kuchukulia usahali juu ya jambo hili na kulifumbia macho na kusema kwamba watu waachwe na kwamba watu wasikimbizwe. Tunasema kwamba sisi hatumkimbizi yeyote. Bali sisi tunawatakia watu kheri na tunataka warudi katika usawa na haki. Hili lina manufaa zaidi kwao katika dini na Aakhirah yao. Ama tukiwaacha juu ya Bid´ah, shirki, kuzikanusha sifa na majina ya Allaah ni kuufanyia ghushi Ummah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: “Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake na kwa viongozi wa Kiislamu na watu wa kawaida.”[1]

[1] Ameipokea Muslim (95) na Abu Daawuud (4944).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 105-106
  • Imechapishwa: 13/11/2018