77. Takbiyr ya pili katika swalah ya jeneza


79- Kisha alete Takbiyr ya pili na amswalie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Umaamah iliyotajwa ya kwamba alikhabarishwa na mmoja katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Sunnah katika swalah ya jeneza imamu alete Takbiyr, kisha asome ufunguzi wa Kitabu baada ya Takbiyr ya kwanza kimyakimya nyepesi, halafu amswalie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), aitakase du´aa juu ya jeneza katika Takbiyr (tatu); asisome chochote katika Takbiyr hizo. Kisha alete Tasliym kimyakimya nyepesi [wakati anapogeuka [upande wake wa kulia]. Sunnah ni wale walioko nyuma yake wafanye mfano wa vile alivofanya imamu wao.”

Ameipokea ash-Shaafi´iy katika “al-Umm” (01/239-240), al-Bayhaqiy (04/39) kutoka katika njia yake, Ibn-ul-Jaaruud (265), kutoka kwa az-Zuhriy, kutoka kwa Abu Umaamah. az-Zuhriy amesema mwishoni mwake:

“Muhammad al-Fihriy amenihadithia, kutoka kwa adh-Dhwahhaak bin Qays ya kwamba amesema mfano wa maneno ya Abu Umaamah.”

ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawasemi jambo fulani kuwa ni Sunnah na haki isipokuwa kwa Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – Allaah (Ta´ala) akitaka.”

Ameipokea al-Haakim (01/360) na al-Bayhaqiy amepokea kutoka kwake isipokuwa yeye amesema: “Wamenikhabarisha watu katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Kilichobaki ni kama mfano wake. Juu yake kuna ziada mbili. Katika mlolongo wa wapokezi wake wa pili amemzidisha “Habiyb bin Mas-lamah” kama ilivyotangulia katika upokezi wa at-Twahaawiy katika masuala yaliyoashiriwa punde kidogo (74). Kisha al-Haakim akazidisha:

“az-Zuhriy amesema: “Abu Umaamah amenihadithia hilo na huku Ibn-ul-Musayyib akisikia na wala hakumkatalia.” Akasema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.” adh-Dhahabiy akaafikiana naye, mambo ni kama walivosema.

Udhahiri wa maneno yake baada ya kutaja kisomo “halafu amswalie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), aitakase du´aa juu ya jeneza katika Takbiyr tatu” ni kwamba kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunakuwa baada ya Takbiyr ya pili na si kabla yake. Kwa sababu ingekuwa kabla yake isingelikuwa imeingia ndani ya Takbiyraat bali kabla yake, kama ambavo mambo yako wazi. Hivo ndivo walivosema Hanafiyyah, ash-Shaafi´iyyah na wengineo tofauti na Ibn Hazm na ash-Shawkaaniy (03/53).

Kuhusu namna ya tamko la kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika jeneza sijaona chochote katika Hadiyth ambazo ni Swahiyh[1]. Kinachodhihiri ni kwamba jeneza haina tamko maalum. Bali ndani yake kunaletwa tamko lolote katika zile namna za matamko yaliyothibiti katika Tashahhud katika swalah za faradhi[2].

[1] Imepokelewa kutoka kwa Ibn Mas´uud namna ya tamko linalokaribiana na swalah ya Ibraahimiyyah. Lakini hata hivyo cheni ya wapokezi wake ni nyonge sana. Kwa hiyo hakuna haja ya kujishughulisha nayo. Ameitaja as-Sakhaawiy katika “al-Qawl-ul-Badiy´”, uk. 153-154, Ibn-ul-Qayyim katika “Jalaal-ul-Afhaam” na akasema:

“Bali imesuniwa kumswalia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika jeneza kama anavomswalia katika Tashahhud. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndivo alivowafunza Maswahabaha zake pindi walipomuuliza namna gani ya kumswalia.”

[2] Nayo ni matamshi aina saba. Nimeyataja katika “Swifatu Swalaat-in-Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Tazama chapa mpya iliyotolewa na Maktabat-ul-Ma´aarif ar-Riyaadh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 154-156
  • Imechapishwa: 02/02/2022