77. Kifo cha Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Aliyafanya haya kwa miaka kumi. Baada ya hapo akafa, lakini Dini yake imebaki.

MAELEZO

Mtume alifanya haya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa miaka kumi baada ya Hijrah. Wakati Allaah alipomkamilishia dini na akaitimiza neema Yake juu ya waumini, ndipo Allaah alimchukua kuwa karibu na Yeye na kukutana na marafiki wa juu – Mitume, wakweli, mashahidi na waja wema.

Alianza kuuguwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwishoni mwa mwezi wa Safar na mwanzoni mwa mwezi wa Rabiy´ al-Awwal. Akawatokea watu hali ya kuwa amevaa kitambaa kichwani mwake na akapanda juu ya minbari. Halafu akasoma shahaadah na kitu cha kwanza alichoanza kutaja baada ya hapo ni kuwaombea msamaha mashahidi wa Uhud. Kisha akasema:

“Allaah amempa khiyari mja miongoni mwa waja Wake kati ya dunia na yaliyo Kwake. Akachagua yaliyo kwa Allaah.”

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) akafahamu anachomaanisha na akaanza kulia na kusema: “Tunawatoa fidia baba zetu, mama zetu, watoto wetu, nafsi zetu na mali zetu kwa akili yako.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Taratibu, ee Abu Bakr.”

 Kisha akasema:

“Ikiwa kuna watu waliyonipa amani kwa usuhuba na mali yake, basi ni Abu Bakr. Ningelimfanya mtu mwingine zaidi ya Mola Wangu kuwa rafiki wa karibu, basi ningelimfanya Abu Bakr. Lakini kuwepo urafiki na mapenzi ya Uislamu.”[1]

Akamwamrisha Abu Bakr aendelee kuwaswalisha watu. Siku ya jumatatu tarehe kumi na mbili Rabiy´ al-Awwal, au kumi na tatu, mwaka wa 11 baada ya Hijrah Allaah akamchukua kuwa karibu Naye. Katika kitanda chake pindi mauti yalipomjia akawa anachukua mkono wake na kuuweka ndani ya maji, halafu anapangusa uso wake na huku akisema:

“Hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Hakika mauti yana machungu.”

 Kisha anaelekeza macho yake juu mbinguni na kusema:

“Ee Allaah! Rafiki wa juu.”[2]

Akafariki siku hiyo. Watu wakavutana na walikuwa na haki ya kufanya hivo. Ndipo alipokuja Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh), akapanda juu ya minbari, akamsifu Allaah na halafu akasema:

“Yule aliyekuwa akimwabudu Muhammad, basi atambue kuwa Muhammad ameshakufa, na yule aliyekuwa akiamwabudu Allaah, basi atambue kuwa Allaah yuhai na hafi.”

Halafu akasoma:

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ

“Na Muhammad si yeyote isipokuwa ni Mtume tu. Wamekwishapita kabla yake Mitume. Je, akifa au akiuawa mtageuka nyuma ya visigino vyenu?” (Aal ´Imraan 03 : 144)

إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ

”Hakika wewe utakufa na wao pia ni  watakufa.” (az-Zumar 39 : 30)

Watu wakaanza kuangua kilio kikali na kukinaika kuwa kweli (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekufa. Akaoshwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndani ya nguo zake kwa ajili ya kumuheshimu. Kisha akavikwa sanda ya pamba kwa nguo tatu nyeupe bila ya kanzu wala kilemba. Kisha watu wakamswalia makundi mbalimbali bila ya imamu.

Baada ya khaliyfah kupewa kiapo cha utiifu na usikivu, akazikwa usiku wa kuamkia jumatano – swalah na amani zimshukie yeye kutoka kwa Mola Wake.

[1] Muslim (2382).

[2] al-Bukhaariy (4449).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 141
  • Imechapishwa: 03/06/2020