76. Uwajibu wa kuhukumu kwa Shari´ah katika Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat


Miongoni mwa mambo yaliyofungamana na masuala haya ni kwamba kuhukumu kwa aliyoteremsha Allaah sio kama jinsi wanavyofahamu baadhi ya watu wanaojinasibisha na ulinganizi eti kwamba inahusiana na kuhukumu katika magomvi ya kipesa na haki mbalimbali peke yake. Hakuna wanayoomba isipokuwa haya tu. Wanasema kwamba kuhukumu kwa aliyoteremsha Allaah ni mahakamani peke yake. Hili ni kweli kwamba ni lazima mahakama yahukumu kwa aliyoteremsha Allaah na kwamba kumaliza magomvi na mizozo kati ya watu inakuwa kwa kutumia Shari´ah. Lakini jambo halikuishilia hapo peke yake. Bali ni wajibu kuhukumu kwa aliyoteremsha Allaah katika mambo ya ´Aqiydah pia, ambayo ndio muhimu zaidi. Watu wametofautiana kwayo. Ni wajibu kuhukumu kait yao kwa aliyoteremsha Allaah na kuwabainishia watu ´Aqiydah sahihi kutokamana na ´Aqiydah batili. Ama kusema ya kwamba watu waachwe waamini watakavyo, kwamba watu wasishtushwe na kwamba kila mmoja aamini atakavyo. Haya ni maneno batili yasiyojuzu. Mwenye kujuzisha kwamba kila mmoja afuate imani inayotaka na kwamba watu wako huru katika ´Aqiydah anaritadi kutoka katika Uislamu.

Ni wajibu ´Aqiydah iwe kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah inapokuja katika Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat.

Ni wajibu kuhukumu kwa aliyoteremsha Allaah katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah kwa njia ya kwamba ´ibaadah zote afanyiwe Allaah na kwamba kumfanyia ´ibaadah mwingine asiyekuwa Yeye ni shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislamu. Ni wajibu kuhukumu kwa haya. Kwani huu ndio msingi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomtuma Mu´aadh kwenda Yemen alimwambia:

“Iwe jambo la kwanza kuwalingania ´kushuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah´.”

Hakumtuka ili atatue mizozo peke yake. Bali alimtuma ili kwanza alinganie katika ´Aqiydah sahihi. Hili pia ndio jambo ambalo walianza nalo Mitume. Walianza kwa ´Aqiydah. Jambo halikomeki juu ya kutatua magomvi peke yake. Bali ´Aqiydah sahihi inatakiwa kubainishwa na ahukumiwe yule anayeenda kinyume na ´Aqiydah sahihi ya kwamba ni kafiri na mshirikina. Mshirika ni mfano wa yule anayemwabudu asiyekuwa Allaah, mwenye kuchinja na akaweka nadhiri kwa asiyekuwa Allaah, mwenye kuwataka msaada wafu. Kwa nini mtu kama huyu aachwe na asihukumiwe? Wanapogombana na mwingine juu ya mbuzi watu wanasema kuwa wahukumiwe kwa yale aliyoteremsha Allaah na wakati huohuo anaachwa juu ya ´Aqiydah yake ijapokuwa atakuwa ni mshirikina. Haijuzu. Ni lazima kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah katika ´Aqiydah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 103-105
  • Imechapishwa: 13/11/2018