76. Hali tano zinazopelekea kutamka au kufanya neno la kufuru

Kwa kifupi ni kwamba yule mwenye kutamka neno la kufuru hatoki katika hali tano:

Hali ya kwanza: Awe anayaamini ndani ya moyo wake. Huyu hapana shaka juu ya ukafiri wake.

Hali ya pili: Awe sio mwenye kuyaamini moyoni mwake na wala hakutenzwa nguvu. Ameyafanya kwa ajili ya maslahi ya kidunia, kuwapaka watu mafuta au kwa kutaka kuafikiana nao. Huyu ni kafiri pia kwa dalili ya Aayah.

Hali ya tatu: Mwenye kufanya kufuru na shirki kwa kutaka kuafikiana na watu wake na wakati huo huo akawa haipendi na wala haiamini moyoni mwake. Ameifanya kwa ajili ya kuilinda nchi yake, mali yake na jamaa zake.

Hali ya nne: Afanye hivo hali ya kufanya mzaha na mchezo, kama walivyofanya wale watu waliotajwa. Huyu anakuwa kafiri kwa dalili ya Aayah tukufu.

Hali ya tano: Aseme hivo kwa kulazimishwa na sio kwa kutaka kwake na wakati huo huo moyo wake uwe umetua juu ya imani. Huyu amepewa ruhusa ya kufanya hivo kwa vile ametenzwa nguvu.

Kuhusu hali nne zilizotangulia mwenye kufanya hivo anakufuru. Hivyo ndivyo zinavyoweka wazi Aayah. Kwa haya kuna Radd kwa wale wenye kusema kuwa mtu hahukumiwi kufuru hata kama atasema neno la kufuru au akafanya neno la kufuru mpaka yajulikane yaliyomo ndani ya moyo wake. Maneno haya ni batili kwani yanaenda kinyume na maandiko. Ni maneno ya Murji-ah wapotevu.

Shaykh (Rahimahu Allaah) ametaja kanuni kubwa kuhusiana na kutenzwa nguvu inayojulisha ni hali ipi mtu anapewa udhuru na ni hali ipi ambayo mtu hapewi udhuru. Amesema:

“Na ni jambo linalojulikana ya kwamba mtu hatenzwi nguvu isipokuwa katika maneno au kitendo. Ama itikadi iliyoko moyoni, hakuna anayetenzwa nguvu kwa hilo.”

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 121-122
  • Imechapishwa: 30/04/2017