76. Amesahau akazungumza ndani ya swalah kwa kusahau

Swali 76: Swalah ya mtu inaharibika akizungumza ndani ya swalah kwa kusahau?

Jibu: Akizungumza muislamu ndani ya swalah kwa kusahau au kwa ujinga swalah yake haibatiliki. Ni mamoja swalah hiyo ni ya faradhi au ya iliyopendekezwa. Allaah (Subhaanah) amesema:

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[1]

Imethibiti katika “as-Swahiyh” kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Nimekwishafanya.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Mu´aawiyah bin al-Hakam as-Sulamiy (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba alimtakia rehema mchemuaji ndani ya swalah kutokana na kujahili kwake hukumu ya ki-Shari´ah ambapo walioko pambizoni mwake wakamkemea kwa kumwashiria. Baadaye akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo na hakumwamrisha kuirudia swalah yake. Msahaulifu ni kama mfano wa mjinga na aula zaidi. Jengine ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizungumza ndani ya swalah kwa kusahau na hakuirudia swalah yake. Bali alikamilisha swalah yake kama ilivyopokelewa katika Hadiyth Swahiyh kupitia kwa Ibn Mas´uud, ´Imraan bin Huswayn na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

Kuhusu kuashiria ndani ya swalah hapana neno ikiwa haja imepelekea kufanya hivo.

[1] 02:286

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 81
  • Imechapishwa: 22/09/2022