75. Uwajibu wa kutambua mambo yanayopingana na Tawhiyd

Lakini ni juu yako kufahamu Aayah mbili katika Kitabu cha Allaah: ya kwanza ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Msitoe udhuru! Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (at-Tawbah 09 : 66)

Ukielewa ya kwamba baadhi ya Maswahabah ambao walipigana vita warumi wakiwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikufuru kwa sababu ya maneno ambayo waliyatamka kwa njia ya utani na mzaha, hapo ndipo itakubainikia ya kwamba yule mwenye kutamka kwa neno la kufuru na akalifanyia kazi kwa kuchelea mali yake isipungue au cheo au kwa sababu anataka kumpaka mtu mafuta, ni jambo baya zaidi kuliko yule ambaye [kakufuru kwa] kuongea kwa maneno ambayo anafanya nayo mzaha. Aayah ya pili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake [yuko hatiani] – isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake umetua juu ya imani, lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake – basi hao wana ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kubwa. Hivyo ni kwa sababu wao wamefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah.” (an-Nahl 16 : 106-107)

Allaah Hakuwapa udhuru watu hawa, isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake umetua juu ya imani. Kuhusu mwengine asiyekuwa huyu, amekufuru baada ya kuamini kwake, sawa ikiwa kafanya hilo kwa ajili ya khofu, tamaa ya kimaisha, kutaka kumpaka mtu mafuta, cheo kwa watu wa nchi yake, jamaa zake au kwa ajili ya mali yake, au kafanya hilo kwa mzaha au sababu zingine miongoni mwa sababu – isipokuwa tu yule aliyelazimishwa. Aayah inafahamisha hivi kwa mitazamo miwili: ya kwanza ni Kauli Yake:

إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ

“… isipokuwa yule aliyelazimishwa… “

Allaah (Ta´ala) hakumvua yeyote isipokuwa tu yule aliyelazimishwa, na ni jambo linalojulikana ya kwamba mtu hatenzwi nguvu isipokuwa katika maneno au kitendo. Ama itikadi iliyoko moyoni, hakuna anayetenzwa nguvu kwa hilo. Ya pili ni Kauli Yake (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“… hivyo ni kwa sababu wao wamefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah.”

Kwa hiyo ameweka wazi ya kwamba kukufuru huku na adhabu sio kwa sababu ya kuitakidi, ujinga, kuichukia dini au kupenda kufuru, isipokuwa sababu yake ni kwa ajili ya kutaka kupata sehemu katika mambo ya dunia na kwa ajili hiyo akayapa kipaumbele juu ya dini.

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Anajua zaidi. Himdi zote anastahiki Allaah, Moal wa walimwengu. Swalah na Salaam zimwendee Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake wote.

MAELEZO

Ukitambua kanuni hii ambayo ni kutambua yanayoipitikia imani sahihi basi itakuwa ni wajibu vilevile kutambua yale maneno au matendo yanayopingana nayo. Katika yale ni kunaingia maneno anayotamka mtu ambayo ni moja katika vitenguzi vya Uislamu ambayo anafanya mzaha kwayo anakufuru. Haijalishi kitu kama hamaanishi kweli katika maneno yake hayo. Katika dini hakuna mzaha. Dalili ya hayo ni kisa cha watu waliotoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk kuwapiga vita Warumi. Ilipomfikia khabari Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Rumi inajipanga kuwashambulia waislamu ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakimbilia katika wakati kulikuwa joto kali, katika majira ya joto, wakati ambapo ulikuwa wa matunda mazuri na masafa yalikuwa marefu kutoka al-Madiynah kwenda Tabuuk. Kulikuwa watu miongoni mwa wale waliotoka pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliokaa sehemu na kuanza kufanya mzaha. Mmojo wao akasema:

“Hatujaona mfano wa wasomaji wetu hawa! Wana matumbo mapana, wanasema uongo sana na ni waoga wakati wa mapambano.”

Wanamaanisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake. Katika kikao kile kulikuwa kijana mmoja katika Answaar ambaye aliwakemea na akamwambia:

“Umesema uongo. Wewe ni mnafiki! Nitamwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Pindi kijana huyu alipoenda kumwambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakuta Wahy umeshamtangulia na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameshateremshiwa maneno Yake (Ta´ala):

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Ukiwauliza watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (09:65-66)

Watu hawa wakaja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoa udhuru na kumwambia kwamba malengo yao ilikuwa ni kupiga porojo tu ili wajirahisishie uzito na urefu wa safari. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuzidisha kitu zaidi ya kuwasomea hiyo Aayah.

Ikiwa watu hawa walimkufuru Allaah na wakaritadi ilihali hapo kabla walikuwa waislamu kwa sababu ya neno walilosema kwa njia ya utani na mchezo, ni vipi kuhusu yule mwenye kutamka neno la kufuru – sio kwa njia ya mzaha – kwa ajili ya kuhifadhi mali, cheo na nafasi yake? Huyu ni muovu zaidi kuliko mwenye kufanya mzaha. Kwa kuwa mtu huyu amefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 120-121
  • Imechapishwa: 28/04/2017