75. Kusoma al-Faatihah na Suurah nyingine katika Rak´ah ya kwanza


77- Kisha baada ya Takbiyr ya kwanza atasoma al-Faatihah na Suurah nyingine[1]. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya Twalhah bin ´Abdillaah bin ´Awf ambaye ameeleza:

“Niliswali nyuma ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) juu ya jeneza ambapo akasoma ufunguzi wa Kitabu [na Suurah nyingine na akasoma kwa sauti mpaka akatusikilizisha. Pindi alipomaliza nikamshika mkono wake na kumuuliza ambapo] akasema: [Nimesoma kwa sauti] ili mjue kuwa ni Sunnah [na ni haki.]”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/158), Abu Daawuud (02/68), an-Nasaa´iy (01/281), at-Tirmidhiy (02/142), Ibn-ul-Jaaruud katika “al-Muntaqaa” (264), ad-Daaraqutwniy (191) na al-Haakim (01/358-386).

Mtiririko ni wa al-Bukhaariy, ziada ya kwanza ni ya an-Nasaa´iy na cheni za wapokezi wake ni Swahiyh. Ibn-ul-Jaaruud katika hizo wametaja Suurah na wawili hao wanayo hiyo ya tatu kwa cheni ya wapokezi Swahiyh, al-Haakim anayo ya pili kutoka katika njia nyingine kutoka kwa Ibn ´Abbaas kwa cheni ya wapokezi ambayo ni nzuri.

Imepokelewa kutoka kwa kikosi cha Maswahabah kuhusiana na maudhui haya. Itakuja Hadiyth ya mmoja wao katika masuala ambayo yatafuatia baada ya haya.

Punde tu baada ya Hadiyth hii at-Tirmidhiy akasema:

“Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh. Ndivo inavofanywa kwa mtazamo wa baadhi ya wanachuoni katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo. Wanachagua kusoma al-Faatihah baada ya Takbiyr ya kwanza. Pia ndio maoni ya ash-Shafi´iy na Ishaaq. Baadhi ya wanachuoni wamesema: “Hakusomwi chochote katika swalah ya jeneza. Kilichomo ni kumsifu Allaah, kumswalia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuombea du´aa maiti. Nayo ndio maoni ya ath-Thawriy na wengineo katika wanachuoni wa Kuufah.”

Hadiyth hii na zengine zilizokuja zikiwa na maana yake ni hoja dhidi yao. Hakusemwi kwamba ndani yake hakujasemwa uwazi kuyanasibisha hayo kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu sisi tunasema: “Maneno ya Swahabah anaposema “Katika Sunnah ni jambo fulani” ni musnadi iliyoegemezwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi mpaka kwa Hanafiyyah. Bali an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´” (05/232):

“Hayo ndio maoni yenye nguvu zaidi yaliyosemwa na wanachuoni wengi katika watu wetu katika msingi na mengineyo katika Usuwliyyuun na Muhaddithuun.”

Ibn Humaam katika “at-Tahriyr” ndivo amekata kauli kwa kuhakiki. Yule ambaye amekifanyia maelezo, Ibn Amiyr Haaj (02/224), amesema:

“Haya ndio maoni ya wenzetu waliotangulia na ndio yamechukuliwa na mtunzi wa “al-Miyzaan” na ash-Shaafi´iyyah na jopo la walio wengi katika Muhaddithuun.”

Juu yake miongoni mwa mambo ya kushangaza ni kuona Hanafiyyah kutoitendea kazi Hadiyth hii, licha ya usahihi wake, kupokelewa kwake kwa namna nyingi na kusilihi kwake, katika kuithibitisha Sunnah kwa mujibu wa njia na misingi yao. Imaam Muhammad amesema katika “al-Muwattwa”, uk. 175:

“Hakusomwi chochote katika jeneza. Haya ndio maoni ya Abu Haniyfah.”

Mfano wake katika “al-Mabsuutw” cha as-Sarakhsiy (02/64):

“Wakati baadhi ya wanachuoni waliokuja nyuma walipoona kuwa maoni haya yako mbali na usawa na kule kupingana kwake na Hadiyth ndipo akasema kuwa inafaa kusoma al-Faatihah kwa sharti mtu ainuilie du´aa na kumsifu Allaah. Wameshurutisha jambo hilo kwa ajili ya kuoanisha – kwa madai yao – kati ya Hadiyth na maoni ya maimamu wao, pamoja na kwamba sharti yenyewe hii ni batili kwa kutothibiti kwake pia inabatilishwa na kule kuthibiti kusoma Suurah nyingine pamoja na al-Faatihah katika Hadiyth, jambo ambalo limekuja kwa kuachia na haiwezekani kuishurutishia sharti hii pia.

Wanao jambo la ajabu jengine ambalo ni kusema kwao:

“Kusoma:

سبحانك

“Kutakasika ni Kwako… “

baada Takbiyr ya kwanza ni katika Sunnah za swalah juu ya jeneza.”

Ingawa ni jambo halina msingi wowote katika Sunnah, kama tulivyotangulia kuzindusha jambo hilo katika maelezo ya chini, uk. 119. Wamekusanya kati ya kuthibitisha jambo lisilokuwa na msingi wowote katika Sunnah na kukataa usuniwaji wa yaliyopokelewa ndani yake.

Ikiwa utasema kuwa mhakiki Ibn Humaam amesema katika “Fath-ul-Qadiyr” (01/459):

“Wamesema: “Hakusomwi al-Faatihah isipokuwa ikiwa ataisoma kwa nia ya kumsifu Allaah na haikuthibiti kusomwa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

maneno haya kutoka kwa mhakiki mfano wa huyu ni ya kushangaza zaidi kuliko yote yaliyotangulia. Kwani kuthibiti kisomo kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni miongoni mwa mambo yasiyofichikana kwa mtu mfano wake pamoja na kwamba yamekuja katika “Swahiyh-ul-Bukhaariy” na vyenginevyo ambavo tumetangulia kuvibainisha. Kwa ajili hiyo ni jambo linalokuwa na dhana yenye nguvu kwamba anaashiria kwa jambo hilo kuwa Hadiyth haiwezi kusimama kama dalili juu ya kuthibitisha kisomo katika swalah ya jeneza kwa kusema juu yake “Sunnah” kutokana na tofauti ambayo tumetangulia kuitaja. Mambo yakiwa hivo tunavofikiria basi haya ni maajabu mengine. Kwani hakika madhehebu yake ni kwamba maneno ya Swahabah ni Sunnah na ni yenye hukumu ya musnadi kilichoegemezwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama tulivyotangulia kuyanukuu hayo kutoka katika kitabu chake “at-Tahriyr”. Hivo ndivo wanavopita katika mambo yao ya mataga. Chukua mfano wa hayo masuala yanayofuata. Amesema katika “al-Hidaayah”:

“Maiti atapobebwa juu ya kitanda basi watakamata juu ya miguu yake minne. Hivo ndivo ilivyopokelewa katika Sunnah. ash-Shaafi´iy amesema: “Sunnah ni kwamba kibebwe na watu wawili; ambaye yuko mbele akibebe begani mwake na wa pili akibebe kifuani mwake.”

Ibn-ul-Humaam amesema katika hali ya kuraddi kile kilichonasibishwa kwa ash-Shaafi´iy:

“Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tofauti na yale waliyoyaendea.”

Kisha akataja kutoka katika njia ya Abu ´Ubaydah kutoka kwa baba yake ´Abdullaah bin Mas´uud ambaye amesema:

“Yule ambaye atalisindikiza jeneza basi akamate pande zote za jeneza. Kwani hivo ndio katika Sunnah.”

Ameipokea Ibn Maajah (01/451) na al-Bayhaqiy (20-194). Ibn Humaam amesema:

“Imewajibika kuhukumu kwamba kitendo hichi ndio Sunnah na kwamba kinyume chake, ingawa imethibiti kutoka kwa baadhi ya Salaf, pengine ni kutokana na hali fulani.”

Tazama namna ambavo amefanya maneno ya Ibn Mas´uud “Katika Sunnah ni jambo fulani” kuwa katika hukumu ya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na sambamba na hilo hakufanya maneno ya Ibn ´Abbaas vivyo hivyo! Je, hivi kweli chimbuko la mgongano huu unatokana na kusahau au ni ushabiki wa kimadhehebu? Allaah atusalimishe kutokamana na hayo.

Haya, endapo tutakadiria yamesihi kutoka kwa Ibn Mas´uud, tusemeje ilihali si sahihi kwa sababu imekatika; Abu ´Ubaydah hajakutana na baba yake kama ilivyotajwa katika “al-Jawhar-un-Naqiyy” ya Ibn-ut-Turkumaaniy al-Hanafiy na kwa ajili hiyo nimepuuzilia mbali kuiweka Sunnah hii inayodaiwa katika kitabu chetu hichi, kama ambavo tumepuuzilia mbali juu ya ile inayokabiliana nayo inayonasibishwa kwa ash-Shaafi´iy kwa sababu ya kutopokelewa kwake.

Isitoshe ziada ya kwanza katika Hadiyth Abu Ya´laa pia ameipokea katika “Musnad” yake, kama ilivyokuja katika “al-Majmuu´” (05/234) ya an-Nawawiy na akasema:

“Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.” al-Haafidhw akamkubalia katika “at-Talkhiysw” (05/165).

an-Nawawiy ametumia hoja kwa ziada hii juu ya kwamba inapendeza kusoma Suurah nyingine fupi. Lakini katika Hadiyth hakuna kinachofahamisha kuwa ni fupi. Pengine dalili ya hilo ni yale yaliyotangulia juu ya kutakikana kufanya haraka kwa majeneza kuyapeleka katika makaburi yake. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] Hapa kuna ishara ya kutosuniwa kusoma du´aa ya kufungulia swalah. Hayo ndio madhehebu ya Shaafi´iyyah na wengineo. Abu Daawuud amesema katika “al-Masaa-Il” yake (153):

“Nimemsikia Ahmad akiulizwa kuhusu mtu anayesoma du´aa ya kufungulia swalah katika swalah ya jeneza ambapo akasema: “Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu… Sijapatapo kusikia.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 151-154
  • Imechapishwa: 01/02/2022