75. Hukumu ya kusafiri kwenda katika miji ya kikafiri

Haijuzu kusafiri kwenda katika miji ya makafiri isipokuwa kwa masharti matatu yafuatayo:

1- Mtu awe na elimu, kiasi cha kwamba itamlinda kutokamana na hoja tata.

2- Mtu awe na dini, kiasi cha kwamba itamzuia matamanio.

3- Mtu awe ni mwenye kuhitajia hilo.

Ikiwa masharti haya hayatotimizwa, basi itakuwa haijuzu kusafiri kwenda katika miji ya makafiri kwa sababu ya fitina, au kuchelea fitina, inayopatikana huko. Isitoshe ndani yake kuna kuiharibu pesa. Kwa sababu safari hizi zinagharimu pesa nyingi.

Hata hivyo ikiwa kutakuwa na haja ya kufanya hivo, kama kwenda kimatibabu au kusoma elimu ambayo haipatikani katika mji wake, na akawa na elimu na dini kutokana na tuliyoyataja, basi hakuna neno mtu akifanya hivo.

Safari za utalii kwenda katika miji ya makafiri hazizingatiwi kuwa ni haja. Isitoshe kuna uwezekano akasafiri kwenda katika miji ya Kiislamu ambapo watu wake wanachunga nembo za Kiislamu. Hii leo baadhi ya miji yetu ya Kiislamu – na himdi zote njema ni stahiki ya Allaah – imekuwa ni miji ya kitalii. Ikiwa mtu ana uwezo badala yake asafiri kwenda huko na kujifurahisha na kutumia likizo yake.

Kuhusu kuishi katika miji ya makafiri, hakika khatari yake ni kubwa juu ya dini, tabia, mwenendo na adabu zake. Sisi na wengine tumeshuhudia kuharibika kwa wengi wanaoishi huko na wakarudi kwa sura nyingine. Wamerudi hali ya kuwa ni watenda madhambi mazito. Baadhi yao wamerudi hali yakuwa ni wenye kuritadi. Hawaamini si dini yao wala dini nyenginezo – na tunaomba kinga kwa Allaah. Wengine wamefikia hali ya kukanusha kila kitu, kuichezea shere dini na watu wake wa zamani na wa sasa. Kwa ajili hio ndio maana ni wajibu kwa kila mmoja kujitenga na hilo na kushikamana na masharti yenye kumzuia mtu na matamanio juu ya sehemu hizo za maangamizo.

Kuishi katika miji ya makafiri ni lazima kupatikane sharti mbili za kimsingi:

1- Yule mtu anayeishi huko awe na amani na uhakika juu ya dini yake, kwa njia ya kwamba awe na elimu na imani. Awe na azma yenye nguvu ambayo itamfanya kuwa na thabati juu ya dini yake na atahadhari na upotevu na upindaji. Vilevile awe na chuki na bughudha kwa makafiri. Asiwafanye kuwa ni marafiki zake au akawapenda kwa sababu kujenga nao urafiki na kuwapenda ni katika mambo yanayopingana na imani. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ

“Hutokuta watu wanaomuamini Allaah na siku ya Mwisho kwamba wanawapenda wale wanaopinzana na Allaah na Mtume Wake – japo wakiwa ni baba zao, watoto wao, ndugu zao au jamaa zao.” (al-Mujaadalah 58 : 22)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا الْيَهُودَ وَالنَّصَارَىٰ أَوْلِيَاءَ ۘ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ فَتَرَى الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ يُسَارِعُونَ فِيهِمْ يَقُولُونَ نَخْشَىٰ أَن تُصِيبَنَا دَائِرَةٌ ۚ فَعَسَى اللَّـهُ أَن يَأْتِيَ بِالْفَتْحِ أَوْ أَمْرٍ مِّنْ عِندِهِ فَيُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا أَسَرُّوا فِي أَنفُسِهِمْ نَادِمِينَ

“Enyi mlioamini! Miswafanye mayahudi na manaswara kuwa ni marafiki – wao kwa wao ni marafiki na yeyote atakayewafanya marafiki, basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah haongoi watu madhalimu. Basi utawaona wale ambao katika nyoyo zao mna maradhi wanawakimbilia wakisema: “Tunakhofu isitusibu mgeuko.” Basi huenda Allaah akaleta ushindi au jambo litokalo Kwake, wakawa wenye kujuta kwa waliyoyaficha katika nafsi zao.” ( al-Maaidah 05 : 51-52)

Imethibiti katika “as-Swahiyh” ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuwapenda watu basi ni katika wao. Mtu yuko pamoja na yule ampendaye.”

Kitu kinachoweza kuwa chenye khatari kubwa kwa muislamu ni yeye kuwapenda maadui wa Allaah. Kwa sababu kuwapenda kunapelekea kukubaliana na wao na kuwafuata. Au angalau kwa uchache ni mtu kutokemea batili zao. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote mwenye kuwapenda watu basi yeye ni katika wao.”

2- Mtu awe na uwezo wa kudhihirisha dini yake. Hili linafanywa kwa njia ya kusimamisha zile nembo za Uislamu pasi na kizuizi. Ikiwa wapo watu wa kutosheleza ili kuweza kusimamisha swalah ya ijumaa na swalah za mkusanyiko, afanye hivo pasi na kuzuiwa. Vilevile asizuiwe kutoa zakaah, kufunga, hajj au mengineyo katika nembo za dini. Ikiwa hawezi kufanya mambo hayo, basi haijuzu kukaa katika nchi hii na hivyo itakuwa ni lazima kufanya Hijrah. Ibn Qudaamah amesema katika “al-Mughniy´ (08/457) wakati alipokuwa anazungumzia watu sampuli mbalimbali juu ya suala la Hijrah:

“Mmoja wapo ni mtu ambaye ni wajibu kwake kufanya Hijrah. Huyu ni yule mwenye kuwa na uwezo wa kufanya hivo na hawezi kudhihirisha dini yake. Hawezi kutekeleza mambo ya wajibu ya dini yake kati ya makafiri. Mtu huyu ni lazima kwake kufanya Hijrah. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ ۚقَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا فَأُولَـٰئِكَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَعْفُوَ عَنْهُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَفُوًّا غَفُورًا

“Hakika wale ambao Malaika wamewafisha, hali ya kuwa wamejidhulumu nafsi zao, wataambiwa: “Mlikuwa katika hali gani?” Watasema: “Tulikuwa tukikandamizwa katika ardhi.”  Malaika watasema: “Je, kwani ardhi ya Allaah haikuwa pana mkahajiri ndani yake?” Basi hao makazi yao yatakuwa ni Moto – na ubaya ulioje mahali pa kurejea! Isipokuwa wale waliokandamizwa kati ya wanaume na wanawake na watoto ambao hawakuweza kupata namna yoyote wala hawawezi kuongoza njia. Basi hao huenda Allaah akawasamehe – na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kughufiria.” (an-Nisaa´ 04 : 97-99)

Haya ni matishio makali kabisa yanayoonyesha kuwa ni wajibu. Kutekeleza wajibu wa dini yake ni lazima kwa yule mwenye uwezo wa kufanya hivo. Na Hijrah ni katika mambo ya wajibu ya dharurah na yenye kuikamilisha. Jambo lolote lisilotimia isipokuwa kwa kufanya jambo hilo, basi jambo hilo litakuwa ni wajibu pia.”

Baada ya kukamilisha masharti haya mawili ya kimsingi, kukaa katika nchi ya kikafiri kumegawanyika vigawanyo mbalimbali:

1- Akae kwa ajili ya kulingania katika Uislamu. Hii ni aina fulani katika jihaad na ni faradhi kwa baadhi ya waislamu wenye uwezo wa kufanya hilo. Hata hivyo kwa sharti Da´wah iweze kufikiwa na kusikuwepo yeyote mwenye kuizuia au kuiitikia. Kwa sababu kulingania katika Uislamu ni katika mambo ya wajibu ya dini na kadhalika ni miongoni mwa mfumo wa Mitume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kufikisha kutoka kwake katika kila zama na mahali. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fikisheni kutoka kwangu ijapokuwa Aayah moja.”[1]

2- Akae huko kwa ajili ya kuzisoma hali za makafiri na kuyajua yale mambo waliyomo katika ´Aqiydah mbovu, ´ibaadah za batili, tabia mbaya na maumbile ya vurugu ili apate kuwatahadharisha watu wasighurike nao na pia awabainishe uhakika wa hali zao wale wenye kupendezwa nao. Sampuli ya ukaaji huu pia ni aina fulani ya jihaad kwa sababu mtu anatadharisha kufuru na watu wake pamoja na kulingania katika Uislamu na uongofu wake. Kuharibika kwa ukafiri ni dalili inayofahamisha juu ya utengemaaji wa Uislamu. Kuna methali inayosema:

Kwa kinyume chake yanapata kubainika mambo.

Sharti ya hili kufanywa ni lazima mtu afikie lengo bila ya hilo kupelekea katika madhara makubwa kuliko hilo lengo. Hata hivyo ikiwa lengo halikupatikana kwa njia ya kwamba akazuiwa kuonyesha yale waliyomo na kutahadharisha nao, hakuna faida yoyote ya kukaa kwake. Lakini ikiwa lengo litapatikana pamoja na madhara makubwa, kwa mfano wakakabiliana naye kwa kuutukana Uislamu, Mtume wa Uislamu na wanachuoni wa Uislamu, basi ni wajibu kusimamisha kazi hiyo. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَسُبُّوا الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ فَيَسُبُّوا اللَّـهَ عَدْوًا بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ كَذَٰلِكَ زَيَّنَّا لِكُلِّ أُمَّةٍ عَمَلَهُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّهِم مَّرْجِعُهُمْ فَيُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Na wala msiwatukane wale wanaowaomba asiyekuwa Allaah wasije nao wakamtukana Allaah kwa uadui pasi na kujua. Hivyo ndivyo tumewapambia kila ummah matendo yao, kisha kwa Mola wao pekee yatakuwa marejeo yao ambapo atawajulisha kwa yale waliyokuwa wakitenda.” (al-An´aam 06 : 108)

Hili linafanana na kukaa katika miji ya kikafiri ili kuwapeleleza kwa ajili ya waislamu ili apate kujua yale wanayoyapanga dhidi ya waislamu na halafu akawatahadharisha waislamu. Ni kama ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma Hudhayfah bin al-Yamaan kwenda kwa washirikina ili apate kujua khabari zao katika vita vya Khandaq[2].

3- Akae huko kwa ajili ya haja ya nchi ya Kiislamu na kupanga mafungamano yake na nchi za kikafiri. Kwa mfano mabalozi. Huyu ana hukumu moja na yule mwenye kukaa kwa ajili yake [hiyo nchi ya Kiislamu]. Kwa mfano yule mwenye kusimamia mambo ya kielimu ambaye anaishi hapo kwa ajili ya kuchunga mambo ya wanafunzi na anawalazimisha kushikamana barabara na dini ya Uislamu, tabia na adabu zake, hivyo kunapatikana manufaa makubwa na wakati huohuo kunaondoka madhara makubwa.

4- Akae huko kwa ajili ya haja maalum na inayojuzu. Kwa mfano biashara na matibabu. Katika hali hii inafaa kukaa huko kadiri na haja. Wanachuoni wamesema kuwa inajuzu kuingia katika miji ya makafiri kwa ajili ya biashara. Wamejengea hoja hilo kutokana na baadhi ya mapokezi ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

5- Akae huko kwa ajili ya kusoma. Aina hii inafanana na ile ya kabla yake. Hata hivyo aina hii ni khatari na inaharibu zaidi juu ya dini ya mtu na tabia yake. Mwanafunzi daima hujihisi kuwa chini ya waalimu zake. Hili linapelekea mtu kuwaadhimisha na kuridhia tabia zao, fikira zao na mienendo yao. Hivyo wakawafuata, isipokuwa yule ambaye Allaah amemuhifadhi – nao ni wachache.

Jengine ni kwamba mwanafunzi huhisi kuwa ni mwenye haja ya mwalimu wake. Hilo linapelekea hatimaye akaanza kumpenda na kumpaka mafuta katika upotevu na upindaji aliyomo.

Vilevile mwanafunzi wakati wa kozi ya masomo anapata wanafunzi wenzake anaowafanya marafiki ambao anawafanya kuwa ni marafiki anaowapenda na akaathirika nao.

Kwa ajili ya khatari hii kigawanyo hichi, ni lazima kwa mtu awe makini zaidi kuliko kile cha kabla yake. Katika hayo masharti mawili ya kimsingi kumeongezwa juu yake masharti mengine mawili ya kimsingi:

1- Mwanafunzi awe na akili iliokomaa sana. Hili tukiwa na maana ya kwamba awe ni mwenye kuweza kupambanua kati ya mazuri na mabaya na awe na uoni wa mbali juu ya mambo yanayokuja huko mbele. Ama kuwapeleka watoto wadogo na ambao hawajakomaa, ni khatari kubwa juu ya dini zao, tabia zao na mienendo yao. Halafu isitoshe ni khatari pia juu ya jamii zao ambao watazirudilia. Pindi watakapowarudilia, basi wanaanza kueneza sumu zao ambazo wamezipata kutoka kwa wale makafiri. Hili limeshuhudiliwa na linashuhudiliwa mpaka hivi leo kutokana na hali ilivyo.

Wengi katika wanafunzi waliotumwa wamerudi wakiwa ni watu wengine. Wamerudi hali ya kuwa wamepotea katika imani zao, tabia zao na mienendo yao. Ni jambo linalojulikana kwamba mambo haya yamewadhuru watu hawa na jamii zao. Kuwatuma watu hawa katika nchi kama hizi ni kama kuitupa mbuzi kati ya mijibwa mwitu.

2- Mwanafunzi awe na elimu kubwa ya kidini, itayomuwezesha kuweza kupambanua kati ya haki na batili na aweze kupambana na batili kwa haki. Hili linahitajika ili asije akadanganyika na batili waliyomo na akafikiria kuwa ni haki, mambo yakamchanganya au akashindwa kuraddi batili na hivyo akabaki hali ya kuwa amechanganyikiwa na akaanza kufuata batili. Kuna du´aa iliyopokelewa inayosema:

اللهم أرني الحق حقاً وارزقني اتباعه، وأرني الباطل باطلاً وارزقني اجتنابه

“Ee Allaah! Nionyeshe haki kuwa ni haki na uniruzuku kuweza kuifuata. Nionyeshe batili kuwa ni batili na uniruzuku kuweza kuiepuka.”

3- Mwanafunzi awe ni mtu mwenye dini itayomuhifadhi na kumlinda kutokamana na kufuru na maasi. Hii ina maana ya kwamba yule mtu ambaye ana imani dhaifu hatosalimika na kukaa katika nchi kama hizo. Isipokuwa yule ambaye Allaah atamsalimisha. Hili linatokana na kuwa mashambulizi ni yenye nguvu na mshambuliwaji ni mnyonge. Sababu za kufuru na maasi ni zenye nguvu na zimejaa katika nchi hizo. Zinapokutana na mtu ambaye nguvu za upinzani wake ni nyonge, basi hufanya kazi zake.

4- Kuwepo haja ya elimu ambayo mwanafunzi amekaa katika nchi hiyo kwa ajili yake. Hili linahitajia ya kwamba elimu yake iwe na manufaa kwa waislamu na masomo kama hayo hayapo katika miji ya waislamu. Ikiwa ni elimu ambayo haina manufaa yoyote kwa waislamu au ambayo ipo tayari katika miji ya Kiislamu, basi itakuwa haijuzu kukaa katika miji ya kikafiri kwa ajili yake. Sababu ya hili ni ile khatari na madhara yanayopatikana katika dini na tabia ya mtu. Sababu nyingine ni mali nyingi inayopotea pasi na faida.

5- Kukaa huko kwa ajili ya kuishi. Aina hii ni khatari na kubwa zaidi kuliko ya kabla yake. Hili linapelekea katika maharibifu ambayo moja wapo ni kule kuchanganyikana kikamilifu na makafiri. Uharibifu mwingine ni kule mtu kuhisi kuwa nchi hiyo ni nchi yake na mtu anakuwa amefungamanishwa na yale mambo yanayopelekea nchi kama mapenzi na urafiki. Mtu anakuwa ni mwenye kuzidisha idadi ya makafiri. Familia yake inakuja kulelewa kati ya makafiri na hivyo wanachukua tabia na ada zao. Huenda wakawafuata wao katika ´Aqiydah zao na ´ibaadah. Kuhusiana na hilo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kukaa na mshirikina na akaeshi naye, basi ni kama yeye.”[3]

Hadiyth hii – licha kwamba cheni ya wapokezi wake ni dhaifu – lakini ina mtazamo upande mmoja. Kule kuishi nao kunapelekea katika kuchanganyika nao. Qays bin Haazim amepokea kutoka kwa Jariyr bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi niko mbali na kila muislamu anayeishi kati ya washirikina.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Kwa nini?” Akasema: “Mmoja katika wao wawili hatakiwi kuona moto wa mwingine.”[4]

Ameipokea Abu Daawuud na at-Tirmidhiy.

Wengi katika wapokezi wameipokea Hadiyth hii kupitia kwa Qays bin Haazim kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kutaja Swahabah yeyote katikati. at-Tirmidhiy amesema:

“Nimemsikia Muhammad – yaani al-Bukhaariy – akisema: “Swahiyh ni Hadiyth ya Qays kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bila ya kutaja Swahabah yeyote katikati.””

Vipi moyo wa muumini utakuwa ni wenye furaha kwa kuishi katika mji wa kikafiri ambapo kunatangazwa ndani yake mambo ya kikafiri na hawahukumu kwa hukumu ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Anaona yote hayo kwa macho yake, anayasikia kwa masikio yake na akaridhia. Bali uhakika wa mambo ni kwamba anajinasibisha na nchi hiyo, anaeshi huko na mke wake na watoto wake na akahisi utulivu ndani yake, kama jinsi anavyohisi utulivu katika miji ya waislamu. Ukiongezea na ile khatari kubwa pia tuliyotaja inayopatikana kwake yeye, mke wake na watoto wake katika dini na tabia zao.

Hapa ndipo tumepofikia juu ya kuishi katika nchi za kikafiri. Tunamuomba Allaah yawe yameafikiana na haki na usawa.

[1] al-Bukhaariy (3461).

[2] Muslim (1788).

[3] Abu Daawuud (2784).

[4] Abu Daawuud (2643) na at-Tirmidhiy (1654).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 131-138
  • Imechapishwa: 03/06/2020