76- Kisha ataweka mkono wake wa kulia juu ya mgongo wa kiganja chake cha kushoto na kifundo na kigasha cha mkono kisha ajikaze juu ya kifua chake. Kumepokelewa Hadiyth kadhaa juu ya hilo ambapo ni lazima nitaje baadhi yake:

Ya kwanza: Abu Hurayrah amesimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth yake iliyotangulia punde kidogo:

“… akaweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto.”

Hadiyth hii, ijapo ni yenye cheni ya wapokezi ambayo ni dhaifu, lakini maana yake ni Swahiyh kwa ushahidi wa Hadiyth zinazofuata ambazo kwa kuachiliwa kwake zinakusanya pia swalah ya jeneza kama ambavo pia zinakusanya swalah zote ambazo sio za faradhi kama mfano wa swalah ya kuomba mvua, swalah ya kupatwa kwa jua na nyenginezo.

Ya pili: Sahl bin Sa´d ameeleza:

“Watu walikuwa wakiamrishwa mtu aweke mkono wake wa kushoto juu ya kifundo chake cha mkono wa kushoto ndani ya swalah.”

Ameipokea Maalik katika “al-Muwattwa” (01/174), al-Bukhaariy (02/178) kupitia njia yake na mtiririko ni wake. Vivyo hivyo Imaam Muhammad katika “al-Muwattwa” (156), Ahmad (05/336) na al-Bayhaqiy (02/28).

Ya tatu: Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza: “Nilimsikia Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakika sisi kongamano la Manabii tumeamrishwa kuharakisha kukata swawm kwetu, kuchelewesha daku yetu na kuweka mikono yetu ya kuume juu ya mikono yetu ya kushoto.”

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (885- Mawaarid), at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” (10851) katika “al-Awsatw” (01/01-10) kupitia njia zao wawili hao na adh-Dhwiyaa´ al-Maqdisiy katika “al-Mukhtaarah” (02/10/63).

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim. as-Suyuutwiy ameisahihisha kaitka “Tanwiyr-ul-Hawaalik” (01/174).

Inayo njia nyingine kutoka kwa Ibn ´Abbas.

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr”, adh-Dhwiyaa´ al-Maqdisiy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Vilevile ina shawahidi zengine nilizozitaja katika takhriyj ya kitabu chetu “Swifatu Swalaat-in-Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ya nne: Twawuus ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto kisha anaikaza juu ya kifua chake akiwa ndani ya swalah.”

Ameipokea Abu Daawuud (01/121) kwa cheni ya wapokezi nzuri kutoka kwake. Hadiyth hiyo, ijapo kuna Swahabah aliyekosekana katika cheni ya wapokezi, lakini ni hoja mbele ya wanachuoni wote. Kuhusu wale ambao wanaijengea hoja moja kwa moja ni jambo liko wazi. Miongoni mwao ni wanachuoni wengi. Ama kuhusu wale wasioitumia kama hoja isipokuwa pale ambapo imepokelewa kwa njia nyingine ambayo imeunganika cheni ya wapokezi wake au iwe na shawahidi – jambo ambalo ndilo la sawa – ni kwa sababu haya yana shahidi mbili:

1- Waa-il bin Hujr ameeleza:

“Kwamba yeye alimuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto kisha akaiweka juu ya kifua chake.”

Ameipokea Ibn Khuzaymah katika “as-Swahiyh” yake kama ilivyo katika “Naswb-ur-Raayah” (01/314) na pia ameipokea al-Bayhaqiy katika “Sunan” yake (02/30) kupitia njia mbili kutoka kwake ambapo moja inaitilia nguvu nyingine.

2- Qabiyswah bin Hubl kutoka kwa baba yake aliyesema:

“Nilimuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akigeuka kuliani na kushotoni mwake na nilimuona – amesema – akiweka hii juu ya kifua chake. Yahyaa (naye ni Ibn Sa´iyd) akasifia kwamba ni mkono wa kuume juu ya mkono wa kushoto juu ya kifundo cha mkono.”

Ameipokea Ahmad (05/226) kwa cheni ambayo wapokezi wake ni waaminifu. Ni wapokezi wa Muslim mbali na huyu Qabiyswah. al-´Ijl na Ibn Hibbaan wamemfanya kuwa mwaminifu. Lakini hakupokea kutoka kwake zaidi ya Simaak bin Harb. Ibn-ul-Madiyniy na an-Nasaa´iy wamesema “Hajulikani.” Katika “at-Taqriyb” imekuja kwamba “Ni mwenye kukubalika.”

Mfano wake Hadiyth yake inakuwa nzuri katika shawahidi. Kwa ajili hiyo at-Tirmidhiy amesema, baada ya kumfanyia takhriyj kutoka katika Hadiyth hii ya kuushika mkono wa kushoto kwa mkono wa kulia:

“Hadiyth ni nzuri.”

Hizi ni Hadiyth tatu juu ya kwamba Sunnah ni kuiweka juu ya kifua[1]. Hatoingiwa na shaka yule mwenye kuangalia mkusanyiko wake ya kwamba inafaa kuzitumia kama hoja katika jambo hilo.

Kuhusu kuweka chini ya kitovu ni dhaifu kwa makubaliano. Hivo ndivo alivosema an-Nawawiy, az-Zayla´iy na wengineo. Nimeyabainisha hayo katika takhriyj iliyoashiriwa punde kidogo.

[1] Katika chapa yangu mpya ya kitabu changu “Swifatu Swalaat-in-Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)”, uk. 12-17 kuna Radd kwa baadhi ya wahafidhina wa Hanafiyyah wa hii leo katika kule kuifanya  kwao kubaya Sunnah hii.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 148-151
  • Imechapishwa: 01/02/2022