c) Baadhi ya wanawake na wasimamizi wao wanachukulia wepesi mwanamke kuingia ndani kwa daktari kwa hoja kwamba eti anahitajia matibabu. Haya ni maovu na khatari kubwa ambayo haijuzu kuikubali na kuinyamazia. Shaykh Muhammad bin Ibraahiym (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Kwa hali yoyote kukaa faragha na mwanamke wa kando ni jambo ambalo Kishari´ah ni haramu. Haijalishi kitu hata kama ni daktari anayemtibu. Hayo ni kutokana na Hadiyth:

“Mwanamume hakai faragha na mwanamke isipokuwa shaytwaan huwa ni watatu wao.”

Ni lazima aandamane na mwengine pamoja naye. Ni mamoja awe mume wake au mmoja katika Mahram zake wa kiume. Isipowezekana japo mmoja katika ndugu zake wa kike ikiwa hakumpata mmoja katika wale tuliyowataja na wakati huohuo ugonjwa ukawa ni wa khatari usiyoweza kucheleweshwa, basi angalau kwa uchache wahudhurie wauguzi wa kike na mfano wao kwa ajili ya kuzuia faragha iliyokatazwa.”[1]

Kadhalika haijuzu daktari wa kiume kukaa faragha na mwanamke wa kando. Ni mamoja daktari wa kike huyo ni rafiki yake au muuguzi wa kike.

Wala pia haifai faragha ya mwalimu kipofu au mwengine pamoja na wanafunzi wa kike.

Wala pia haifai faragha ya mwanamke muhudumu ndani ya ndege pamoja na mwanamume ambaye ni wa kando naye. Watu wameyachukulia wepesi mambo haya kwa jina la utamaduni wa uwongo, kuwafuata kichwa mchunga makafiri na kuzipuuza hukumu za Kishari´ah. Hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah, Aliye juu, Aliyetukuka.

Wala haijuzu mwanamke mwenye nyumba kukaa faragha na mfanyakazi wa kiume ambaye anafanyakazi nyumbani kwake. Tatizo la mfanyakazi ni tatizo la khatari ambalo watu wengi wamepewa kwalo mtihani katika zama hizi kwa sababu ya kuwashughulisha wanawake na masomo na kazi nje ya majumba. Mambo hayo yanalazimisha juu ya waumini wa kiume na waumini wa kike kushika tahadhari ipasavyo na kuchukua hatua zilizo salama ambazo ni za lazima. Hawatakiwi kwenda pamoja na mila ambazo ni mbaya.

[1] (10/13).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 126-127
  • Imechapishwa: 12/12/2019