Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) atawalipa waja Wake waumini maradufu.

MAELEZO

Siku ya Qiyaamah Allaah atawalipa waja Wake kwa matendo yao:

وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا

“Na Mola wako hamdhulumu yeyote.”[1]

Kila mmoja atalipwa kwa matendo yake aliyofanya; yakiwa ni mema basi atalipwa mema, na yakiwa ni maovu atalipwa uovu. Matendo mema ambayo waumini waliyafanya duniani watalipwa kwayo maradufu kutokana na fadhilah za Allaah:

مَنْ جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا

“Atakayekuja kwa tendo jema basi huyo atapata thawabu kumi mfano wake.”[2]

Jema moja linalipwa kuanzia mara kumi mpaka mara miasaba na zaidi ya hivo kiasi kinachojua Allaah pekee. Haya ni katika fadhilah Zake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Wale waliofanya madhambi yaliyo chini ya shirki na kufuru, basi Allaah ima akawaadhibu kwayo kwa kiwango cha madhambi hayo au akawasamehe. Haya yanawahusu waumini peke yao. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[3]

Kwa msemo mwingine ni kwamba ima akawasamehe au akawaadhibu ndani ya Moto kisha baadaye akawatoa ndani yake na badala yake kuwaingiza Peponi. Hali hii inahusiana na madhambi makubwa yaliyo chini ya shirki.

[1] 18:49

[2] 6:160

[3] 04:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 57
  • Imechapishwa: 12/08/2021