74. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya hodhi ya Mtume


Mwandishi (Rahimahu Allaah) amesema

wala [usipinge] hodhi na mizani – hakika wewe unanasihiwa

La pili: Hodhi. Inahusu hodhi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni jambo limepokelewa kwa mapokezi mengi ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko na hodhi. Urefu wake ni mwendo wa mwezi na upana wake ni mwendo wa mwezi. Maji yake ni meupe sana kuliko maziwa na ni matamu zaidi kuliko asali. Vikombe vyake ni idadi ya nyota zilizoko mbinguni[1]. Itaendewa na Ummah wake, wanywe humo na atazuiwa kila mzushi na kila mwenye mashaka. Mwenye mashaka atazuiwa na wala hatomwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Atapouliza sababu ya kuzuiwa – yaani hawa wenye mashaka – ataambiwa:

“Ni kwa sababu hawakuacha kuendelea kuwa ni wenye kuritadi kwenye visigino vyao.”[2]

Kwa watu aina ya pili – yaani kuhusu wazushi – ataambiwa:

“Hakika wewe hujui yale waliyoyazua baada yako.”[3]

Kila ambaye alizua Bid´ah katika dini, kama Mu´tazilah, Khawaarij, Shiy´ah na mapote mengine ya upotevu ambayo yamezua ndani ya dini yasiyokuwemo watazuiwa na hodhi siku ya Qiyaamah. Atazuiwa kila mzushi na kila mwenye mashaka na dini yake. Hakuna wataoifikia isipokuwa watu wa imani ya kweli walio imara juu ya imani ya kweli duniani na wakafa juu yake. Hawa ndio wataifikia hiyo hodhi na watakunywa kutoka humo kiasi cha kwamba hawatohisi kiu tena baada yake. Hii ndio hodhi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (6579) na Muslim (27) na (2292)

[2] al-Bukhaariy (6593) na Muslim (26) na (2293)

[3] al-Bukhaariy (6576) na Muslim (28) na (2294)