72. Nasaha za Imaam Ibn Abiy Daawuud

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

ولا تُنكِرَنْ جهلاً نكيراً ومُنكراً

29 – Usimpinge kwa ujinga Nakiyr na Munkar

Bi maana usipinge kitu usichokijua. Sio kila usichokijua unakipinga. Unachotakiwa ni kuamini yale yaliyosihi na kuthibiti hata kama hutoyajua na kuyadiriki. Amesema (Ta´ala):

بَلْ كَذَّبُوا بِمَا لَمْ يُحِيطُوا بِعِلْمِهِ وَلَمَّا يَأْتِهِمْ تَأْوِيلُهُ ۚ كَذَٰلِكَ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ

“Bali wamekadhibisha yale wasiyoyaelewa vyema elimu yake na wala haujawafikia uhakika wake halisi.” (10:39)

Lililo la wajibu ni muumini aamini yale yaliyosihi kutoka kwa Allaah na Mtume Wake ingawa hakuyajua na kuyafikiria. Hakika jambo hilo lina wakati wake litatokea:

لِّكُلِّ نَبَإٍ مُّسْتَقَرٌّ ۚ وَسَوْفَ تَعْلَمُونَ

“Kwa kila habari ina wakati wake maalumu na mtakuja kujua.” (06:67)

Maelezo na simulizi mnazoelezwa kila kitu kina wakati wake. Utapofika wakati wake kitadhihiri. Wajibu wetu ni sisi kukiamini. Kwa sababu ni maneno ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) ambayo:

لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ

“Haitokifikia ubatili mbele yake na wala nyuma yake.” (41:42)

Vilevile ni maneno ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye hazungumzi kwa matamanio yake:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

“Na wala hatamki kwa matamanio yake. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.” (53:03-04)

Tusitegemee akili zetu. Inapokuja katika mambo yaliyofichikana tunatakiwa tutegemee Wahy wenye kuteremshwa na wala tusiingize akili na fikira zetu.

Mambo ya ndani ya kaburi yanahusiana na mambo ya Aakhirah. Endapo tutamfukua mtu baada ya kuwekwa ndani ya kaburi lake tutamkuta kama alivyowekwa. Lakini yuko katika hukumu za ulimwengu mwingine na yale yanayompitikia hatuyaoni na wala hatuwezi kuyahisi. Si kwa jengine ni kwa sababu yuko katika ulimwengu mwingine uliyofichikana kwetu.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Nakiyr na Munkar.”

Haya ni majina ya Malaika wawili wanaomjia maiti pale tu anapofukiwa. Roho yake inarudishwa kiwiliwilini mwake halafu wanamkaza hai. Inahusiana na uhai wa ndani ya kaburi na si kama mfano wa uhai wa ardhini. Ni uhai wa Aakhirah na mwingine asioutambua yeyote isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Wanaitwa hivi kama ilivyotajwa katika Hadiyth isiokuwa na neno katika cheni ya wapokezi wake[1]. Ni majina yaliyothibiti. Kwa sababu muonekano wa Malaika wawili hawa ni wenye kutisha na mtu atawakana na kufazaika nao. Watamjia kwa sura ambayo alikuwa haijui katika uhai wake. Hii ndio sababu wameitwa Munkar na Nakiyr. Hapa kuna Radd kwa wale wenye kupinga majina haya na kusema kuwa ni kuwatukana Malaika. Tunasema kuwa sio kuwatukana Malaika. Hili ni kwa sababu yule watayemjia atawakana. Ndio maana wakaitwa Munkar na Nakiyr.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hakika wewe unanasihiw.”

Bi maana unanasihiwa usiyapinge mambo haya. Dini ni kupeana nasiha. Hivi ndivyo alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: “Ni kwa nani?” Akasema: “Ni kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na kwa watu wa kawaida.”[2]

Mtunzi (Rahimahu Allaah) anasema kwamba anakunasihi usipinge yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), katika Qur-aan na katika Sunnah. Mu´tazilah na wapotevu ambao wanategemea akili na fikira zao wameyapinga hayo. Tahadhari na mwenendo wao na fuata maandiko. Amini yaliyokuja katika maandiko sahihi. Huku kunaingia katika kumuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] at-Tirmidhiy (1071) na at-Twabariy katika “al-Mu´jam al-Awsatw” (05/44). at-Tirmidhiy amesema:

“Ni nzuri (Hasan) na geni.”

[2] Muslim (95) na (55)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 161-163
  • Imechapishwa: 12/01/2024