Hakika baadhi ya wanawake na wasimamizi wao wanachukulia wepesi kwa aina mbalimbali za ukaaji faragha ikiwa ni pamoja na:

a) Mwanamke kukaa faragha pamoja na ndugu zake mume pamoja na kuacha wazi uso wake mbele yao. Faragha hii ina khatari zaidi kuliko nyingine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tahadharini na kuingia sehemu za wanawake.” Mtu mmoja katika Answaar akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unasemaje kuhusu al-Hamuu.” Akajibu: “al-Hamuu ni kifo.”

Ameipokea Ahmad, al-Bukhaariy, at-Tirmidhiy na akaisahihisha.

Maana ya al-Hamuu ni yule ndugu yake mume. Kama kwamba alichukia kukaa naye faragha. al-Haafidhw bin Hajar amesema katika “Fath-ul-Baariy”:

“Wanachuoni wa lugha wameafikiana juu ya kwamba al-Ahmaa´ (mashemeji) ni wale ndugu zake mume wa mke; kama baba yake mume, kaka yake mume, mtoto wa kaka yake, mabinamu na mfano wao.” Akasema tena: “Makusudio katika Hadiyth ni wale ndugu zake mume – mbali na wale baba zake na watoto wake; kwa sababu hao ni Mahram zake mke na inafaa kwao kukaa naye faragha na hawaitwi kuwa ni kifo – kimazowea ilivyo ni kwamba hawa wanachukuliwa wepesi. Matokeo yake mke anakaa faragha na kaka yake mume na hivyo ndio maana akafananishwa na kifo. Huyu ndiye ana haki zaidi ya kukatazwa.”[1]

ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl-ul-Awtwaar”:

“Maneno yake “al-Hamuu ni kifo” bi maana kuwa na khofu juu yake ni kubwa kuliko kwa mwengine. Kama ambavyo khofu juu ya kifo ni kubwa zaidi kuliko juu ya kitu kingine.”[2]

Kwa hiyo basi, ee dada wa Kiislamu, mche Allaah na wala usichukulie wepesi jambo hili ikiwa wengine watafanya hivo. Kinachozingatiwa ni vile inavosema hukumu ya Kishari´ah na sio walivyozowea watu.

[1] (09/331).

[2] (06/122).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 124-125
  • Imechapishwa: 11/12/2019