72. al-Qummiy upotoshaji wake wa tisa wa Aal ´Imraan

al-Qummiy amesema pindi alipokuwa akifasiri Aayah:

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُوا بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

“Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu. Bali wahai kwa Mola wao wanaruzukiwa. Wanafurahia kwa aliyowapa Allaah kwa fadhila Zake na wanafurahi [kwa bishara wale] ambao [bado] hawajaungana nao walio nyuma yao kwamba hakutokuwa na khofu juu yao na wala hawatohuzunika.”[1]

“Baba yangu amenieleza, kutoka kwa al-Husayn bin Mahbuub, kutoka kwa Abu ´Ubaydah al-Hadhdhwaa´, kutoka kwa Abu Baswiyr, kutoka kwa Abu ´Abdillaah aliyesema: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba inawahusu wafuasi wetu pindi watapoingia Peponi na kukutana na karama kutoka kwa Allaah. Wanafurahi juu ya ndugu zao duniani ambao bado hawajaungana nao:

أَلَّا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

“… kwamba hakutokuwa na khofu juu yao na wala hawatohuzunika.”

Aayah hii inawaraddi wale wanaopinga thawabu na adhabu baada ya mauti.”[2]

Allaah amemtakasa Abu ´Abdillaah kutokamana na madai haya ya Raafidhwah. Tunachoamini sisi ni kwamba hajikatii Pepo juu ya nafsi yake mwenyewe, sembuse hawa viumbe waovu kabisa Raafidhwah Baatwiniyyah.

Allaah amemtakasa Abu ´Abdillaah kutokamana na uongo huu mkubwa ambao haijuzu yakasemwa na yeyote isipokuwa Mitume peke yao. Mitume tu ndio wanaweza kusema hivo baada ya kuteremshiwa Wahy kutoka kwa Allaah. Abu ´Abdillaah hawezi na wala hana haki ya kujikatia kuingia Peponi, seuze kuwakatia hawa wapotevu wakubwa, waongo na maadui wakubwa kabisa wa Maswahabah wa Muhamamd (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Aayah inawahusu Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wenye kuuawa katika njia ya Allaah kama waliouawa katika vita vya Badr, kisima cha Mu´uunah na Hunayn na wengine wote ambao wana ´Aqiydah moja kama wao. Ni wale wanaopigana katika wapwekeshaji na wenye nia safi kwa ajili ya Allaah na ili neno la Allaah liweze kuwa juu. Yanayonasibishwa kwa Abu ´Abdillaah ni uongo wa wazi kutoka kwa Raafidhwah hawa waongo ambao hata hawaiamini hiyo Jihaad kwa ajili ya Allaah. Hawapigani ili kulinyanyua neno la Allaah liwe juu. Wakipigana vita basi ni kwa ajili ya matamanio na upotevu wao.

[1] 03:169-170

[2] Tafsiyr al-Qummiy (1/127).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 111-112
  • Imechapishwa: 13/04/2017